Minong'ono ya maandamano wakati Tanzania ikiadhimisha siku ya muungano
Leo hii Tanzania inaadhimisha miaka 54 tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuunda Tanzania.
Lakini nchi imekuwa ikitawaliwa na mazungumzo kuhusu maandamano dhidi ya Rais wa Tanzania Dokta John Magufuli ambayo yamepangwa kufanyika leo.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, mwanaharakati wa kwenye mitandao ya kijamii, mtanzania ambaye makaazi yake ni nchini Marekani amekuwa akiratibu maandamano kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Mange Kimambi amekuwa akiitisha maandamano nchi nzima dhidi ya rais Magufuli kwa kile anachodai kuwa amekuwa akikiuka haki za binaadam na kudidimiza uhuru wa kisiasa nchini
Mara baada ya kuingia madarakani, rais Magufuli alipiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa.Alisema uchaguzi umekwisha sasa ni wakati wa kuchapa kazi.
Ofisi ya mambo ya nje ya Uingereza imewatahadharisha raia wake walio Tanzania kuhusu vurumai ambazo huenda zikatokea.
Katika maandamano ya mwezi Februari, makabiliano kati ya Polisi na waandamanaji yalisababisha kifo cha mwanafunzi mmoja, baada ya risasi ya risasi ya moto kufyatuliwa.
Kutokana na serikali kuweka kutahadharisha umma dhidi ya maandamano, wengi hawana hakika kama maandamano hayo yatafanyika.
Tayari watu kadhaa wamekamatwa wakihusishwa na upangaji wa maandamano hayo.
- Marufuku za utawala wa Rais Magufuli Tanzania
- Watu 7 wakamatwa kuhusiana na maandamano Tanzania
- Uingereza yatoa tahadhari kwa raia wake Tanzania
Mwezi uliopita katika mkutano wa hadhara,rais Magufuli ameonya kuwa watakaoandamana watamtambua.
''Kuna watu walioshindwa kufanya siasa za kweli wangependa tufanye maandamano barabarani kila siku. Nimesema acha waandamane na wataona mimi ni nani''.
Serikali imekana shutuma kuwa imekuwa ikikandamiza uhuru wa upinzani na uhuru wa kujieleza.
Post a Comment