Header Ads

Mkwasa: Mimi si mtu wa kwanza kuwa Katibu Mkuu Yanga


Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwasa, ametolea ufafanuzi uwepo wa taarifa zinazoeleza kuwa wadhifa wake umekalia kuti kavu.

Mkwasa alisema kuwa hakuna tatizo lolote lililopo ndani ya klabu, bali ni mitandao tu imekuwa ikiandika kila wanalolijua.

Kauli hiyo imekuja mara baada ya kuenea kwa taarifa zinazoeleza kuwa Mkwasa anaweza akaachia ngazi ya Ukatibu Mkuu ndani ya Yanga, baada ya kuhusishwa na kuondoka kwa Kocha George Lwandamina.

Kupitia kipindi cha Michezo cha EFM Radio, jana jioni, Katibu huyo pia alisema Yanga imeshakuwa na viongozi wengi, yeye si Katibu wa kwanza kuanza kazi pale, walikuwepo wengi na wakaondoka.

"Mimi si mtu wa kwanza kuwa Katibu Mkuu Yanga, walikuwepo wengi waliokalia kiti hiki lakini hawapo kwa sasa, kama wakati wangu ukifika wa kuondoka, nitaondoka na atakuja mwingine" alisema Mkwasa.

Mbali na hayo, Mkwasa amewataka Wanayanga wote kuwa watulivu katika kipindi hiki ili kuepusha ujio wa migogoro ambayo inaweza ikaleta mtafaruku ndani ya klabu, ambapo hivi sasa wanasubiri mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wolaiita Dicha FC.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.