Zungu amcharukia Mbunge wa Chadema
MWENYEKITI wa Bunge, Mussa Zungu, amemzuia Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza, kuchangia bungeni baada ya kuendelea kulitaja jina la Rais wakati wa kuchangia kwake licha ya kukatazwa kufanya hivyo.
Upendo alikuwa akimhusisha Rais na kuzuiwa kwa maandamano nchini na matangazo ya moja kwa shughuli za chombo hicho cha kutungwa sheria, yaani ‘Bunge Live’.
Kutokana na mbunge huyo kumtaja Rais katika mchango wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, aliomba kutoa taarifa ya kukiukwa kwa kanuni za 68(1) na 64(1) za Bunge akieleza kuwa Rais anawakilishwa na mawaziri ndani ya Bunge kwa mujibu wa Katiba.
“Na kanuni hii ya 64 inatukumbusha kwamba, haturuhusiwi kuzungumza mwenendo wa Rais na hasa anapokuwa katika madaraka ndani ya ofisi yake,” alisema.
Mhagama pia alisema hawatakiwi kuzungumza jina la Rais kutaka kushawishi namna ya kutoa uamuzi na kwamba kama Peneza anaona kuna shida azungumze na wawakilishi wake.
Akitoa majibu ya mwongozo huo, Zungu alisema kuwa jina la Rais halipaswi kutajwa kwa dhihaka, halaumiwi wala hatakiwi kusemwa kama alivyofanya Peneza.
Alimtaka mbunge huyo kuuliza utendaji wa mawaziri kwa kuwa kanuni inawataka wabunge kutohoji utendaji wa Rais ndani ya Bunge.
“Jina la Rais halitumiwi kwa namna ulivyokuwa unalitumia na kwa hiyo, nayafuta maneno yote kwenye hansard (kumbukumbu rasmi za Bunge),” alisema.
Hata hivyo, baada ya kupewa nafasi ya kuendelea kuchangia, Peneza aliendelea kusema juu ya kauli za Rais.
Kutokana na hali hiyo, Mhagama alisimama tena kutaka kutoa taarifa lakini Zungu alimzuia akisema: “Natumia kanuni ya 73 ukae chini hutazungumza tena.”
Wabunge wengine waliochangia walitaka Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura), kuongezewa mgawo wa fedha za bajeti kwa kuwapa nusu ya fedha za Wakala wa Barabara (Tanroad) ili kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi (CCM), alisema kama Tarura haijaongezewa bajeti yake, utakuwa ni wakala ambao umeanzishwa lakini haujaleta tija.
“Sasa hivi wakala huu umeazima watumishi kutoka halmashauri, wapewe watumishi wao na fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara ili ziweze kupitika,” alisema.
Mbali na Mbunge huyo wabunge wengine waliochangia sula hilo ni pamoja na Magdalena Sakaya (Kaliua-CUF), Livingstone Lusinde (Mtera- CCM), Fred Mwakibete (Busokelo-CCM) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini - CUF).
Post a Comment