RC SANARE AFANYA ZIARA SOKO KUU MANISPAA MOROGORO , ATOA MAELEKEZO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, akizungumza na Waandishi wa habari mra baada ya kumalizika kwa ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara wa Soko Kuu la Manispaa ya Morogoro.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akitoa taarifa ya Soko hilo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga (katikati) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare mara baada ya ziara hiyo kumalizika, (kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare,akikagua Vizimba na bidhaa pamoja na kuongea na Wafanyabiashara wa Soko hilo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akitoa maelekezo kwa wafanyabiashara wa Soko hilo.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare, akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Januari 12,2021, amefanya ziara ya kutembelea Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ili kuona na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiasaha wa soko hilo.
Hatua ya Loata Sanare kutembelea soko hilo akiwa pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imekuja baada ya malalamiko kutoka kwa wafanybiashara wa soko hilo kwa madai tofauti tofauti.
Moja ya Changamoto kubwa zilizojitokeza na kuelezwa na baadhi ya wafanyabiashara wakati wa ziara yake ni pamoja na vizimba vingi vya soko hilo kubaki bila wafanyabiashara ilhali kuna wafanyabiashara wengi wakihitaji vizimba hivyo.
Aidha, uwepo wa tozo kubwa kwa kila kizimba kwa mwezi imekuwa ni kero kwa wafanyabiashara hao ambapo kizimba kimoja kwa wafanyabiashara wadogo kimekuwa kikilipiwa shilingi 70,000 kwa mwezi badala ya shilingi 20,000 kwa mwezi bei ambayo imepangwa na Halmashauri hiyo.
Changamoto nyingine ni wateja kuwa wachache kufika sokoni hapo, soko kuwa mbali na kituo cha daladala hivyo wateja kupata changamoto kufika sokoni hapo na kukosekana kwa uzio katika soko hilo ni moja ya kero kunahatarisha usalama wa wafanyabiashara na mali zao.
Chanagamoto nyingine ni baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa zao nje ya soko hivyo kuzuia wateja kuingia ndani ya soko ili kuwafikia wafanyabiashara wenye vizimba wanaouza bidhaa kama hizo zinazouzwa nje ya soko.
Baada ya Mkuu huyo wa Mkoa kutembelea soko na kupokea kero za wafanyabiashara hao, alitoa maelekezo kwa wahusika ikiwa ni pamoja na kushughulikia kero zote zilizojitokeza.
RC Sanare, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msullwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama ndani ya Wilaya kufuatailia kwa kina utaratibu wa ugawaji wa vizimba vya soko hilo kama ulifuata taratibu zote na unafuata makubaliano ya maamuzi ya vikao halali katika ugawaji wa vizimba hivyo.
’’Mkuu wa Wilaya unavyo vyombo vya kuthibitisha hilo,hakikisha hizi changamoto zote na malalamiko yanayotolewa na wafanyabiashara hawa ufumbuzi unapatikana, " Amesema Sanare.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba ameeleza faida ya soko hilo itakayopatikana mara baada ya kuanza rasmi kutumika pamoja na kujibu kero ya tozo la kizimba kuwa kiwango hicho kimefuata uhalisia na gharma ya ujenzi wa soko.
Pia, Lukuba ametaja faida nyingine ya soko hilo ni Kuongezeka kwa mapato ya ndani kutoka 48 Mil kwa mwezi kabla halijavunjwa soko hadi 172.9 Mil kwa mwezi ambapo kwa mwaka soko hilo linatarajiwa kukusanya Shilingi Bil 2.07.
Kwa upande wake Nataria Shirima amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uongozi wa soko hilo kuwakataza wafanyabiashara wa bidhaa za rejareja kufanya biashara mchanganyiko hali inayopelekea mazingira ya upatikanaji wa kodi kuwa mgumu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara wamemuomba Mkuu wa Mkoa Loata Ole Sanare kushusha kodi ya pango kwa wafanyabiashara kulingana na mzunguko mdogo wa wa biashara ilivyo kwa sasa.
Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro limegharimu zaidi ya shilingi 17 Bil. hadi kukamilika kwake. Bil 10 zikitolewa na Serikali Kuu na Bil. 7.5 zikitolewa na benki ya dunia.
Post a Comment