Header Ads

DIWANI LUKOBE AZINDUA KIVUKO MTAA MANYUKI, AAHIDI KUTATUA KERO ZAIDI ZA BARABARA.

 








DIWANI wa Kata ya Lukobe, Mhe. Selestin Mbilinyi, amezindua Kivuko Cha Barabara ya Dr Mbuya  Mtaa wa Manyuki Kata ya Lukobe Manispaa Morogoro  kilichogharimu kiasi Cha Shilingi Milioni 5. 

Uzinduzi huo umefanyika leo Januari 23/2021 katika Mtaa wa Manyuki.

 Akizungumza na Waandishi wa Habari na Wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo fupi ya uzinduzi, amesema kivuko hicho kilikuwa kilio Cha muda mrefu Cha wakazi wa Manyuki. 

Mhe. Mbilinyi, amesema wakati wa Mvua eneo hilo lilikuwa korofi sana na kusababisha Watu pamoja na magari kutopita katika Eneo hilo. Amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Kivuko hicho, kitapelekea Sasa kuunganisha Mitaa na kufanya barabara hiyo kupitika kwa urahisi.

 " Leo tumezindua Kivuko chetu ambacho kimegharimu Shilingi Milioni 5, katika fedha hizo Kuna nguvu ya Wananchi pamoja na Mimi kuchangia, lakini niseme tu , zipo changamoto nyingi za vivuko katika Kata yangu , kikubwa tumeanza na hiki lakini hizi ni nguvu za Wananchi, niwaombe Wananchi wa Mitaa mingine yenye changamoto Kama hizi waunganishe nguvu ili tuanze kufanyia kazi" Amesema Mhe. Mbilinyi.

Mwisho , amemshukuru na kumpongeza Mkurugenzi Manispaa Morogoro Sheilla Lukuba pamoja na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood, kwa uchapakazi na kujali maendeleo hususani katika huduma za elimu. 

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Manyuki, Rashidi Mohamed, amempongeza Mhe. Diwani, huku akiwaomba Wenyeviti wa Mitaa mingine kushirikisha Wananchi katika kuchangia maendeleo. 

Hata hivyo, Alpheo Mbuya, ambaye ni mwananchi wa Mtaa wa Manyuki, amesema suala la maendeleo sio la mtu mmoja bali ni la Wananchi wote. 

Amesema Kama Wananchi watakuwa kitu kimoja Basi maendeleo yatakuwa kwa kasi. Naye Frola Muhando, mwananchi wa Mtaa wa Manyuki, amemshukuru Mhe. Diwani kwa uwajibikaji wake na ufuatiliaji wa changamoto za Wananchi.

 "Kwa kweli Diwani wetu anafanya kazi, ana muda mchache lakini tunaona jitihada zake, kikubwa sisi Wananchi tuendelee kumpa ushirikiano katika kuleta maendeleo Kata yetu ya Lukobe"Amesema Mhando.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.