Header Ads

MANISPAA MOROGORO YATEKELEZA AHADI YA KUKABIDHI BAJAJI 3 ZENYE THAMANI YA MILIONI 24 LAKI 6 KWA VIKUNDI VYA WALEMAVU NA WANAWAKE

               

              

              

              

              

            

           


KATIKA  kuhakikisha kuwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu vinaimarika kiuchumi Manispaa ya Morogoro imetoa  mkopo wa Bajaji 3  wenye thamani ya shilingi milioni 24 na laki 6  kwa vikundi vya wanawake,  na Walemavu.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi mikopo hiyo iliyofanyika nje ya Uwanja wa Mpira wa Miguu Jamhuri Januari 12/2021 ambapo mikopo hiyo ilishatolewa kipindi cha nyuma,  Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Rutahiwa John,  ameipongeza Manispaa kwa kutii agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 kutoka mapato ya ndani kuwezesha wanawake, Vijana  na walemavu.

Amesema kuwa lengo la Serikali kutoa mikopo kwa makundi hayo ni kuhakikisha inawainua wajasiriamali kutoka katika hatua moja ya maendeleo kwenda hatua nyingine na ndio maana imeamua kutoa riba katika mikopo hiyo.

Rutahiwa, amewataka wajasiriamali kuwa makini na kuhakikisha kuwa malengo yao yanatimia kwa kutumia mkopo huo kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha,  amesema kuwa mikopo inayotolewa na Manispaa haiangalii itikadi za dini, siasa wala kabila hivyo kila mmoja ana haki ya kupata mkopo ili mradi awe amekidhi vigezo.

‘Hii mikopo ilishatolewa, lakini tunachokifanya ni kuonyesha Jamii kwamba mikopo hii ipo kwa kutekeleza agizo la Mkurugenzbi wa Manispaa ya Morogoro ya kutaka Mikopo yote ikiwamo Bajaji na Bodaboda zinazotolewa ziwe na lebo ya Manispaa zikionyesha kwamba vyombo hivyo vimeokana na Mkopo wa asilimia 10 ya uwezeshaji wa kiuchumi,niwaombe huu mkopo mlioupata mkautumie kulingana na mpango wa kikundi chenu ili muweze kurejesha kwa wakati na wenzenu waweze kukopeshwa.” Amesema Rutahiwa .

Naye, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Tungi, Mwanitu Sembogo, akitoa shukrani baaada ya kikundi chake kupatiwa mkopo, amewaasa wanavikundi hao kutumia mkopo kwa maendeleo na kuwataka wanawake kutokubali kurubuniwa na waume zao kwa kuwapatia fedha hizo hali itakayopelekea  kutorejesha fedha kwa wakati. Pia amewataka kutotumia fedha hizo kurejesha madeni ya kwenye vikoba.

Kwa upande wa Afisa Mandeleo ya Jamii Kata ya Sultan Area, Maria Matandula, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuwa mstari wa mbele wa kuyasaidia makundi hayo muhimu katika kuelekea uchumi wa Viwanda na kujikwamua na umasikini.

Akiongea kwa niaba ya vijana wenzake , Francis Christian, kutoka Kikundi cha New Vision Disability kutoka Kata ya Tungi,  ameushukuru uongozi wa Manispaa kwa kuwapatia mkopo na kuahidi kufanya kazi kwa bidi ili waweze kurejesha kwa wakati.

Vikundi ambavyo vimekabidhiwa Bajaji hizo vikiwa na lobo ya Manispaa ya kuonyesha Bajaji hizo zimetokana na Mkopo wa Manispaa ni pamoja na Kikundi cha Walemavu cha New Vision Disability-Tungi, MorogoroHopeful Living- Sultan Area cha Walemavu na Neema Tushikamane cha Wanawake -Sulatan Area.

Ikumbukwe kwamba mikopo hiyo ya Bajaji  ilishatolewa tangia mwaka 2020 Julai na ksuhindwa kutolewa kutokana na baadhi ya taratibu kutokukamilika ikiwemo agizo la Mkurugenzi  wa Manispaa ya Morogoro ya kutaka Mikopo yote ikiwamo Bajaji na Bodaboda zinazotolewa ziwe na lebo ya Manispaa zikionyesha kwamba vyombo hivyo vimeokana na Mkopo wa asilimia 10 ya uwezeshaji wa kiuchumi ili wananchi waone mikopo hiyo ipo na Serikali inatekeleza kwa vitendo.


 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.