Header Ads

WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA NA KUHIFADHI MAZINGIRA

Afisa Mazingira na Usafishaji , Samwel Subi.akiwa katika mahojiano katika kituo cha redio ya  Sauti ya Uzima akielezea suala la usafi na tozo ya ada.

Meneja wa Mapato Kampuni ya Kajenjere, Oswini Mwaitete, akizungumza juu ya ratiba za usafi katika maeneo ambayo wamepewa kwa ajili ya usafishaji.


WANANCHI wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro,  wametakiwa kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi mazingira ili yawe endelevu kwa vizazi vijavyo.

Hayo yamesemwa na Afisa Mazingira na Usafishaji , Samwel Subi, leo Januari 27/2021, akiwa katika mahojiano na vituo vya redio Sauti ya Uzima na Planet FM  kwa nyakati tofauti tofauti akielezea suala la usafi na tozo ya ada.

Subi, amesema kuwa  lipo tatizo la uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ambazo ni pamoja na uchomaji misitu, kilimo cha kuhamahama, utupaji taka ngumu hovyo, uharibifu wa vyanzo vya maji na uchomaji mkaa hovyo.

Pia alizitaja athari zinazotokana na shughuli hizi za kibinadamu kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, kupungua na kunyeesha kwa mvua bila mpangilio na kusababisha mafuriko, kutokea kwa ukame, na kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko mfano kipindupindu.

“Hivyo niwasihi wananchi wa Manispaa ya Morogoro , kuhakikisha wanatunza na kuifadhi mazingira ikiwa ni pamoja kuacha kutupa taka hovyo, kuwa na vichaka katika maeneo yanayowazunguka, kufanya shughuli za kibinadamu na vitu vyote vinavyoweza kuchafua mazingira  , " Amesema Subi.

Vilevile amewataka Wananchi wametakiwa kuhakikisha wanafanya usafi wa mazingira na kuzingatia agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la usafi wa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Mwisho, Subi, amewataka Wananchi kulipa tozo ya ada ya taka bila kukosa, kwani malipo hayo ni kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa ya Morogoro za mwaka 2019.

Naye, Mwenyekiti wa Vikundi vya usafi Manispaa ya Morogoro , Kibwana Nkasi, amesema kwa sasa kuna haja ya kutoa elimu ili  Kuongeza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa mazingira mazuri kwa maisha ya viumbe na maendeleo.

Amesema suala la usafi ni jukumu la kila mtu, hivyo katika kutatua baadhi ya matatizo hayo kunatakiwa elimu juu ya kupinga shughuli rafiki na mazingira na Kuelemisha umma juu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kuwa ni wajibu wa kila mmoja, si serikali, vyombo vya habari, taasisi za serikali au zisizo za Serikali, kila mmoja ana  anawajibika  kuyatunza Mazingira.

Naye Meneja wa Mapato Kampuni ya Kajenjere iliyopewa mdhabuni wa usafishaji wa Mji  katika Kata 12 za Manispaa ya Morogoro, Oswini Mwaitete, amesema  kuwa wananchi wanatakiwa kuelimishwa juu ya  umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwani baadhi yao wanategemea misitu kama njia ya kupatia kipato. 

Amesema wao kazi yao ni kuhakikisha wanafanya usafi katika maeneo ambayo walikubaliana , hivyo jukumu pekee la mwananchi ni kuhakikisha kwamba analipa tozo ya ada ya usafi.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.