Header Ads

POLEPOLE ATAKA ZOEZI LA UHAKIKI WA VIZIMBA VYA WAFANYABISHARA SOKO KUU MANISPAA YA MOROGORO KUANZA UPYA.

 

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood (kushoto), Mhe. Polepole (wapili toka kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa (watatu toka kushoto), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga (wapili toka kulia) wakiwa katika ziara.

                                                                                                                                                                                                                                                                     

                                                                                                               
                     
      
                    



                            

KATIBU wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa  na Mbunge wa kuteuliwa, Mhe. Humphrey Polepole, ameuagiza Uongozi wa Wilaya ya Morogoro kuanza upya zoezi la uhakiki wa Vizimba vya Wafanyabiashara walisajiliwa katika Soko hilo ili kubaini wenye sifa na wasio na sifa.

Kauli hiyo ameitoa Januari 10, 2021 , wakati wa Ziara ya kusikiliza na kutatua kero katika Soko hilo mara baada ya kukagua miradi ya maendeleo  inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano katika Manispaa ya Morogoro na mradi wa SGR ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Akizungumza na Waandishi wa Habari ,  Mhe. Polepole, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kwa kushirikiana na Mstahiki Meya , Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro na Ofisi ya CCM Wilaya  kwa kutumia Kamati hiyo ya Soko waanze kufanya uhakiki upya wa wafanyabiashara waliosajiliwa katika Soko hilo ili kubaini wale wenye sifa na wasio nasifa.

“Nataka zoezi hili la uhakiki wa kizimba kwa kizimba kwa kila  mfanyabiashara ili kuhakikisha kweli ni mtu mmoja na kizimba kimoja, nafahamu watu waliomba vizimba, vioski na fremu za biashara , na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro alielekeza  na kukumbusha kwamba ikifika tarehe 5 Januari , 2021, kila mwenye kizimba awe amefika eneo lake, hivyo kwa tarehe aliyotangaza Mkurugenzi ni kwamba leo tarehe 10, sasa tunawatakia kilalakheri wale wenye vizimba ambao hawajafika katika eneo lake, lakini miundombinu ya eneo hili ni kubwa sana lakini Soko hili ni kama ndoo ya maji ina jaa tungetamani kila mtu awe hapa lakini haiwezekani”” Amesema Mhe. Polepole.

Mhe. Polepole ,  ametoa maelekezo kwa Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwamba kwa wale waliokosa eneo katika Soko hili, na hakuna wale walioshika vizimba viwili  waweke utaratibu mzuri ili hao waliokosa wapatiwe maeneo ambayo wataweza nao kufanya biashara zao.

Mwisho, amewahadharisha wale wenye tabia ya kupangisha vizimba kwa mfanyabiashara mwengine kuacha tabia hiyo kabla ya sheria kuchukua hatua kali.


Kwa upande wa  Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amesema hawatawavumilia wale watakaokutwa wana vizimba zaidi ya viwili kwani licha ya kuwa na kero za msingi na manung’uniko lakini kuna haja ya kuangalia kwa jicho pana Changamoto hizo ili pande zote ziweze kuwa kitu kimoja kwa maendeleo ya Manispaa ya Morogoro.

“ Ni kweli kuna changamoto nyingi katika Soko letu, kuna hoja za msingi za wafanyabiashara wa ndani na nje, tumejitahidi kupunguza kero lakini hatukuzimaliza, kama alivyosema mwenezi sasa tunakwenda katika hatua kubwa, hili ni kweli lina changamoto nyingi, lakini tumejitahidi kupunguza kero,lakini nimetengeneza timu kubwa ya kushughulikia kero hizi tunaimani tutazimaliza taratibu taratibu, wiki inayoanza kuanzia tarehe 11 Januari kamati itakuwa hapa kumsikiliza kila mdau  lakini nawaomba tuwe wakweli na kuwa waaminifu katika jambo hili ” Amesema DC Msulwa.

DC Msulwa, amesema  lazima kazi ifanyike kwakuwa fedha zilizojengea Soko hilo ni za walipa kodi.


 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.