SIKU YA UKIMWI DUNIANI, MEYA KIHANGA AWAHIMIZWA WANANCHI KUJITOKEZA KUPIMA AFYA .
SIKU YA UKIMWI DUNIANI, MEYA KIHANGA AWAHIMIZWA WANANCHI KUJITOKEZA KUPIMA AFYA .
Posted On: December 1st, 2019
Desemba mosi dunia inaadhimisha siku ya Ukimwi. Haya ni maadhimisho ya 31. Ni siku inayotumiwa na wanaharakati na wakuu wa nchi, kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi, kupiga vita unyanyapaa na kuhimiza watu kwenda kufanya vipimo ili kufahamu hali zao.
Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri zilizoadhimisha maadhimisho hayo kwa kuzingatia mkakati wa kitaifa wa 90,90,90 ikiwa na maana ya asilimia 90 ya watu wote wanaoishi na VVU na UKIMWI wawe wamejua hali zao za maambukizi ifikapo 2020,Asilimia 90 ya pili ya watu wote waliogundulika kuwa na maambukizi ya VVU na UKIMWI wawe kwenye tiba na matunzo ifikapo 2020 na asilimia 90 ya wote wanaotumia ARV wawe na kiwango cha chini cha virusi ifikapo 2020.
Akisoma risala mbele ya Mgeni Rasmi mratibu wa kudhibiti UKIMWI Manispaa Upendo Elias ,ameeleza kuwa katika asilimia 90% ya kwanza Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro imejikita katika upimaji wa VVU katika Vituo vya afya na katika ngazi ya Jamii kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI na VVU waliopo, upimaji wa VVU unafanyika kwa kulenga wateja ambao wapo katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi ya VVU na UKIMWI kama Wajawazito, Wenza na wateja walioko kwenye dawa (ARV), Watoto chini ya miaka 5 waliozaliwa na Wamama wenye maambukizi ya VVU na UKIMWI, Wanaojidunga , wanaofanya biashara ya ngono na Wagonjwa waliolazwa.
Aidha, ameeleza katika asilimia 90% ya pili, shughuli zinazofanyika ni kuhakikisha wateja wote waliogundulika na maambukizi wana hakikiwa wafikapo CTC na kuanzishiwa ART ndani ya siku 7 na wateja kuelekezwa juu ya ufuasi mzuri na matumizi sahihi ya dawa za kufubaza Virusi (ARV).
Katika asilimia 90 ya tatu, shughuli zinazofanyika ni kuhakikisha kuwa wateja wote waliofikisha miezi 6 wanachukuliwa damu na kupimwa wingi wa Virusi.
Hata hivyo Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Bi Upendo, ameeleza kuwa Manispaa ya Morogoro inajumla ya Vituo 50 vinavyotoa huduma ya upimaji wa VVU na UKIMWI, Kati ya hivyo vituo 16 vinatoa huduma ya tiba na matunzo (CTC), na vituo 43 vinatoa huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto.
Kwa takwimu za Julai, 2018 hadi Juni 2019 Jumla ya wateja waliopima VVU ni 99564, kati yao Wanaume ni 37074 na Wanawake 62490.
Katika idadi hiyo, waliokutwa na maambukizi ya VVU jumla walikuwa 4550 wakiwemo Wanaume 1561 na Wanawake 2989, ambapo kiwango cha maambukizi ni sawa na asilimia 4.5% kwa wateja waliopimwa kwa asilimia 0.5 ukilinganisha na kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018 ambapo kiwango cha maambukizi kwa waliopimwa kilikuwa sawa na asilimia 4.0
Katika hatua nyingine Bi Upendo amesema, kwamba licha ya kuwepo na takwimu hizo na harakati mbali mbali za kudhibiti maambukizi mapya ya VVU wanakabiliwa na changamoto kama vile muitiko mdogo wa upimaji wa wenza wa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI, Wateja kutofika kwenye huduma pindi wanapogundulika na maambukizi, Wateja kutokuhudhuria tiba na matunzo kwa tarehe sahihi walizopangiwa pamoja Wateja kupotea kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ya Siku ya Ukimwi duniani kwaniaba ya Mhe.Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Abdulaziz Abood, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro,Mhe. Pascal Kihanga, amesema licha ya kupata mualiko wa kuwa mgeni rasmi amefurahishwa na maadhimisho hayo jinsi yalivyopendeza na kuwapa pongezi wale wote walioshiriki katika maandalizi na kufanikisha kufanyika kwa shughuli hiyo.
Meya Kihanga amesema kwa kufuata kauli mbiu ya siku ya maadhimisho inayosema "Jamii ni Chachu ya Mabadiliko Tuungane kuzuia maambukizi mapya " amewataka wananchi kutambua umuhimu wa kujua hali zao za afya na kujitokeza kwa wingi katika vituo vya afya na kupima afya zao.
Aidha Meya Kihanga amesema Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani hutoa fursa ya kutathimini hali halisi na kutoa mwelekeo kuhusu udhibiti wa VVU na UKIMWI kuanzia kwenye Mitaa kupitia kamati za kudhibiti UKIMWI Ngazi ya Mtaa, Kata na Halmashauri pamoja na kusisitizia uhai wa kamati hizo kwa malengo mahususi.
Hivyo, ametoa wito kwa wadau wote wanaojishughulisha na mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kuchangia sehemu ya bajeti zao ili kusaidia Halmashauri kufufua kamati hizo.
"Manispaa ya Morogoro ina asilimia 4.5 ya maambukizi ya VVU na UKIMWI, licha ya kukumbushana na kuchukua hatua mbali mbali za kudhibiti lakini siku ya leo ni muhimu sana kwani inatoa fursa ya kutafakari kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika vita dhidi ya VVU na UKIMWI na kubaini changamoto , mafanikio na kuja na mikakati mbali mbali itakayosaidia katika mapambano dhidi ya vita hii"Amesema Mhe. Kihanga.
Kwa upande mwengine, amesema kuwa katika kupambana na kupunguza maambukizi ya VVU na UKIMWI hakuna budi kuhamasisha jamii hasa Vijana waliopo katika maneo ya mitaani kuachana na matumizi ya dawa za Kulevya ambayo nayo huchangia kwa kiasi kikubwa maambkizi ya VVU.
Akihitimisha hotuba yake, amezidi kuwashukuru wadau wote walioshirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba Maadhimisho hayo yanafanyika ambao ni TACAIDS,USAID,Boresha Afya Southern Zone,JHpiego sauti project,JHpiego AIDS Free,THPS,JSI,NACOPHA, NACP na HACOCA.
Post a Comment