Header Ads

Serikali kuimarisha JWTZ zaidi


SERIKALI imesema itaendelea kuliimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kutoa mafunzo, mazoezi ya kijeshi, kulipatia zana na mitambo ya kisasa na kuimarisha miundombinu ya kimkakati ili kupambana na matishio mapya ya kiusalama.

Matishio hayo ni ugaidi, uharamia, biashara haramu za dawa za kulevya, uhamiaji haramu na usafirishaji haramu wa binadamu.

Pia, imesema imelipatia Jeshi la Polisi vitendea kazi muhimu vikiwamo vifaa vya mawasiliano na uchunguzi vitakavyoliwezesha kupambana na majambazi na matukio mengine ya kihalifu.

Mipango hiyo ya serikali ilibainishwa jana bungeni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipowasilisha hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka ujao wa fedha 2018/19.

Majaliwa alisema hatua hiyo italiwezesha jeshi kutekeleza majukumu yake ya ulinzi wa mipaka ya nchi.

Alisema kuwa katika kupambana na matukio mapya ya kiusalama, JWTZ inashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, mamlaka za kiraia na mataifa mengine.

Alisema jeshi hilo limeendelea kudumisha ushirikiano na nchi nyingine kupitia mafunzo ya pamoja na operesheni za kikanda na kimataifa chini ya Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mafaita (UN).

Ili kutekeleza majukumu ofisi yake katika mwaka ujao wa fedha, Majaliwa aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh. bilioni 124.9.

Kati yake, Sh. bilioni 66.1 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 58.7 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, aliliomba Bunge kuidhinisha Sh.  bilioni 125.5 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge kwa mwaka ujao wa fedha. Kati yake, Sh. bilioni 117.2 ni za matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 8.3 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.