WAWEZESHAJI WA VIKUNDI VYA KIJAMII (CCI) WAGAWA VIFAA VYA KUJIKINGA NA CORONA SHULE ZA MANISPAA YA MOROGORO.
Wanafunzi wa Shule za Msingi Azimio A na B Kata ya Kihonda Manispaa ya Morogoro , wakionesha furaha baada ya kukabidhiwa majaba ya maji na sabuni kwa ajili ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA. |
UONGOZI wa Shirika lisilo la serikali la Uwezeshaji wa Vikundi vya Kijamii (Tanzania Urban Poor Federation-TUPF) kupitia Center For Community Initiatives (CCI) wamegawa vifaa tiba ikiwamo Majaba 10 yenye ujazo wa lita 60 kila moja na sabuni za kunawia mikono kwenye baadhi ya Shule za Msingi Manispaa ya Morogoro ikiwa ni moja ya kurudisha gawio kwa jamii .
Zoezi hilo la ugawaji wa vifaa hivyo vya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA,limefanyika leo Julai 14,2020 katika Shule 3 za Msingi Manispaa ya Morogoro ikiwamo Shule ya Msingi Kihonda Majaba 3, Shule za Msingi Azimio A na B Majaba 5 , pamoja na Shule ya Msingi Kiegea Majaba 2.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mratibu wa Tafiti Jamii Kitaifa katika Kaya Masikini (TANZANIA URBAN POOR FEDERATION- TUPF), ambaye pia ni Katibu wa Jukwaa la kuwawezesha Wanawake kiuchumi Mkoa wa Dar Es Salaam, Bi. Husna Seif Shechonge, amesema lengo la kutembelea Shule hizo ni pamoja na kugawa vifaa vya kujikinga na Corona na kuangalia changamoto za wanafunzi hususani suala la Vyoo.
“Tunajua CORONA imepita kutokana na maombi ya Watanzania na jinsi Mhe. Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli ,alivyo tutoa hofu, lakini kupitia ugonjwa huo tumejifunza kwamba kunawa mikono kuna refusha maisha na ni msaada mkubwa kwa afya zetu, kwahiyo tumewaletea watoto vifaa hivi kuendelea kurithisha watoto wetu utamaduni wa kunawa mikono licha ya kutokuwepo na ugonjwa tuna kila sababu ya kuendelea kufuata maelekezo na kuzingatia ushauri wa Wataalamu wetu wa afya pamoja na Viongozi wetu wa Juu katika kujikinga na ugonjwa huu wa CORONA “Amesema Shechonge.
Licha ya kugawa vifaa vya CORONA lakini lengo jengine ni kujifunza na kuona changamoto zinazowakabili wanafunzi shuleni hususani suala la Vyoo wanavyovitumia shuleni kama ni rafiki kwao.
Shechonge, amesema baada ya kuona hali ya vyoo katika Shule walizotembelea , amesema changamoto wamezibeba kama shirika na kuziwasilisha katika ngazi ya Kitaifa kupitia FEDERATION ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kuzifanyia kazi kwani asilimia kubwa ya shule wanafunzi ni wengi matundu ya Choo ni machache.
Naye mthamini na mfuatiliaji shughuli za Center For Community Initiatives (CCI), Stella Stephen, amesema kitendo cha kusaidia vifaa vya kujikinga na CORONA vinatoa mwanya kwa Serikali kuzitumia fedha zilizo katika bajeti ya kununua vifaa tiba na kuziingiza katika matumizi mengine.
Stella, amesema kama elimu ya kunawa mikono itajengewa utamaduni kwa Watanzania wote na watoto shuleni wakielewa zaidi , Tanzania itatengeneza kizazi bora chenye kujua usafi na usalama wa afya katika ustawi wa Jamii na kupelekea Jamii kuishi katika maisha bora .
Kwa upande wa Mratibu wa FEDERATION Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji wa Kiuchumi Wanawake Manispaa ya Morogoro , Bi Edina Hamisi, amesema licha ya ugawaji wa ndoo lakini wamekuwa wakijihusisha sana na Ujenzi wa Vyoo kwa Jamii ambapo mwaka 2010 walifanikiwa kujenga jumla ya Vyoo 100 katika Kata 4 Manispaa ya Morogoro kupitia Center For Community Initiatives na ushirikiano wa Manispaa ya Morogoro chini ya Mkurugenzi Simbei ambaye ndiye aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro.
Licha ya Ujenzi wa Vyoo lakini walifanikiwa kuingiza Maji katika Kata 3 Manispa aya Morogoro ambapo jumla ya watu 80 waliweza kuhudumiwa na kunufaika na mradi huo wa maji.
“Yapo mengi CCI inafanya lakini kwa hili la kupata ugeni kutoka CCI na wana Federation ni moja ya kitendo cha kumuunga Mkono Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kupambana na Ugonjwa wa Corona, ndoo hizi zitawekwa vyooni ili wanafunzi wanapotoka chooni wanawe mikono na ndoo nyengine zitawekwa kwenye maeneo ya kuingilia wanafunzi ili wanapotoka nyumbani wananawa na kuingia shuleni , tunashukuru sana Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kupitia Mkurugenzi Sheilla Lukuba kwa kutukarimu sana ndani ya Manispaa yake, Uongozi wa Shule , Uongozi wa Kata ya Kihonda kupitia Afisa afya, Wanavikundi vya jamii pamoja na Wanafunzi kwani zoezi letu limeenda vizuri na tunaamini yale tuliyoyaona kama Shirika tuna yabeba na kwenda kuangalia jinsi ya kuyafanyia kazi “ Amesema Bi. Edina.
Upande wa Kaimu Afisa afya Manispaa ya Morogoro, Nobert Bilaba, ameupongeza Uongozi wa CCI na FEDERATION kwa kuiungua mkono Manispaa ya Morogoro kwa upande wa Shule katika kupambana na ugonjwa wa CORONA.
“”Tunawashukuru sana, huu ugonjwa unaua, kwa kitendo mlichokifanya mmetusaidia kuwalinda wanafunzi wetu na waalimu wao, sisi Manispaa tunapambana sana na ugonjwa huu na shule zetu zipo salama tumekuwa wafuatiliaji sana wa kutoa maelekezo , lakini niwaombe wanafunzi mmepewa vifaa hivi ambavyo vimetumia gharama kubwa kununuliwa , mvitunze ili viweze kuendelea kuwasaidia na mnapotoka chooni hakikisheni mnanawa mikono, sio kuepuka na CORONA pekee bali hata magonjwa ya milipuko kama vile Homa ya kuhara pamoja na kipindupindu” Amesema Bilaba.
Post a Comment