DC MSULWA AKUNWA NA UJENZI WA CHOO CHA MTOTO WA KIKE MANISPAA YA MOROGORO.
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amefurahishwa na Ujenzi wa Choo cha Mfano cha Mtoto wa Kike kilichopo Shule ya Sekondari TUBUYU Kata ya Boma.
Kauli hiyo ameitoa leo Julai 01, 2020 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Choo hicho kilichojengwa na Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Msulwa, amesema katika miradi ya kijamii ambayo imemfurahisha na kumvutia tangia aanze kazi katika Wilaya ya Morogoro mradi wa Ujenzi wa Choo cha Mfano cha Mtoto wa Kike huku akisema kuwa Choo hicho kitasaidia sana kumwekea mazimgira mazuri mtoto wa kike awapo shuleni.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Choo cha mfano cha Mtoto wa Kike, DC Msulwa, ameambatana na Mkurigenzi wa Manispaa ya Morogoro, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Tungi, maafisa wa idara mbalimbali Manispaa ya Morogoro, Wakuu wa Idara na vitengo Manispaa ya Morogoro, wananchi , waalimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tubuyu.
“Tunafahamu tatizo la vyoo katika shule zetu ni kubwa sana kwani watoto ni wengi na matundu ya vyoo ni machache, hivyo nitoe wito kwa wadau wengine waliopo ndani ya Halmashauri hii pamoja na Wilaya ya Morogoro kwa ujumla kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ili watoto wetu wajisitiri katika vyoo safi na salama," Aliongeza DC Msulwa.
DC Msulwa, amewashukuru sana Baraza la Madiwani, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro pamoja na wataalamu wote wa Manispaa ya Morogoro, huku akiwataka wasiishie hapo badala yake waendelee kujenga vyoo vyenye hadhi hiyo ili kumhifadhi mtoto wa kike.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba amesema tafiti mbalimbali zimefanyika kuhusiana na sababu za mahudhurio hafifu ya Mtoto wa Kike darasani kutokana na vyoo visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana au watoto wakike.
"Tunashukuru sana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Mstaafu Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya na ngazi ya Kata, wataalamu wa Manispaa pamoja na watumishi wote wa Manispaa ya Morogoro kwa kufanikisha ndoto hii ambayo ilikuwa ni tamko la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kutaka kila Shule ijenge vyoo vya Mtoto wa Kike ili kumstiri, na kuwezesha kufanikisha wazo hili, tutaendelea kushirikiana nao, lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba tunaunga mkono juhudi zozote zile ambazo zinaondoa umasikini wa mtanzania au mwananchi wa kawaida, pamoja na kuwaondolea adha Wanafunzi wa kike wanapoingia katika hedhi " Amesema Lukuba.
Lukuba, amesema kuwa licha ya Mtoto wa kike pekee kupata huduma hiyo , pia hawakuawaacha watu wenye ulemavu kwani katika ujenzi huo umezingatia watu wenye changamoto hiyo ya ulemavu kwa kuwatengea choo chao kwa ajili ya kujisaidia ili kuhakikisha mtoto wa kike anahifadhiwa katika choo chenye hadhi na cha mfano.
"Wanafunzi wa Kike wanakabiriwa na changamoto mbalimbali lakini hiki choo ni moja ya safari yetu kwa Manispaa yetu ya Morogoro, lakini bado tuna malengo ya kuendelea kujenga vyoo vyengine vya mfano kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kadri tutakavyojaliwa ili tuendelee kumkomboa Mtoto wa Kike" Ameongeza Lukuba.
Licha ya hapo, Lukuba,amesisitiza wanafunzi waweke nguvu katika masomo na mambo mengine wawaachie wazazi wao wahangaike nayo lakini wakati huo huo waepukane na vishawishi vitakavyoweza kuwakatishia masomo yao na kutotimiza malengo.
Naye Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro, Dr Janeth Barongo, amesema pamoja na kuwa na Choo cha mfano lakini hata kwenye ufaulu wanatakiwa kuwa wamfano .
'"Msome sana Wanafunzi, Choo cha mfano lakini tunataka matokeo ya ufaulu pia yawe ya mfano, lakini kubwa zaidi msome kwa bidii na kuachana na mambo ambayo hayapo katika umri wenu,tunataka matokeo mazuri, mkituonesha hayo tutapata nguvu nasisi ya kuendelea kuwapa vitu vizuri zaidi ya hivi" Amesema Dr Barongo.
Choo hicho cha mfano kina jumla ya matundu ya choo 12 ikiwamo moja kwa ajili ya Watu wenye ulemavu na kimegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 35 zilizotokana na mapato ya ndani ya Manispaa.
Post a Comment