MAAFISA ELIMU KATA, WALIMU WAKUU WA SHULE WATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, akisaini kitabu cha wageni katika Shule ya Msingi Kikundi wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya shule .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba (kulia) , akizungumza na Wanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Kikundi wakati wa kujitambulisha kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Loata Sanare ya kukagua maendeleo ya shule .
Maafisa Elimu Kata na Walimu wakuu wa Shule za Msingi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wametakiwa kutimiza wajibu wao kwa kusimamia kikamilifu ufundishaji ili kuinua kiwango cha ufulu wa Wanafunzi Shuleni.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, leo Julai 02,2020 wakati wa ziara ya kukagua shule pamoja na maandalizi yaliyofanywa baada ya kufunguliwa kwa shule hizo.
RC Sanare, amesema ni jukumu la walimu Wakuu wa shule na Maafisa Elimu Kata kufanya ufuatiliaji wa karibu wa walimu ili kuhakikisha kuwa walimu hao wanatekeleza majukumu yao ya Ufundishaji vipindi mbalimbali Darasani kikamilifu.
Amesisitiza kuwa hatosita kumchukulia hatua za kinidhamu Mwalimu mkuu,ama afisa Eimu Kata yoyote atakaethibitika kushindwa kutekeleza majukumu yake ya usimamizi na ufuatiliaji wa maendeleo ya Elimu katika eneo lake.
'"Nawaagiza Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule hakikisheni kuwa walimu wanafundisha kikamilifu na kumaliza mada mbalimbali zinazofundishwa mashuleni ili kuwawezesha wanafunzi kujiandaa na mitihani kikamilifu, lakini kubwa zaidi hakikisheni kuwa mnadhibiti utoro mashuleni kwa kuhakikisha mnafuatilia kwa karibu Wanafunzi wanaoonekana kutofika shuleni pasipo kuwa na sababu za msingi""Amesema RC Sanare.
Katika hatua nyingine , RC Sanare, amewasisitiza Maafisa Elimu Kata na walimu wakuu wanadhibiti mimba za utotoni kwa kudumisha nidhamu kwa wanafunzi ili kuwanusuru watoto wa kike na athari za mimba za utotoni ambazo zimekuwa tishio kwa wanafunzi hao kutokana na kukatiza masomo.
Amesema ni jukumu la Maafisa Elimu Kata walimu wakuu wa shule na Wanajamii kwa ujumla kukemea tabia ya baadhi ya Wanaume wanaojihusisha na mapenzi na wanafunzi hali inayopelekea wanafunzi hao kukatiza masomo kwa kuishia kubeba uja uzito.
Amewataka Waalimu kutoa taarifa za Wanafunzi wajawazito kwenye mamlaka husika ili kusudi Serikali iweze kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaojihusisha na vitendo viovu vya kuwakatiza wanafunzi wa kike masomo yao.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuwachukulia hatua kali za kinidhamu baadhi ya Watendaji wanaonekana wanakwenda kinyume na utaratibu na sheria za kazi.
""Sisi tunafanya kazi kwa kuwahudumia wananchi, tunapokuja hapa sio kama hatuna kazi nyengine, lakini mbaya zaidi unafika eneo husika unaambiwa Mtendaji ana kazi nyengine, huu sio utaratibu ni nidhamu mbovu sana, wale ambao hawakufika katika mkutano wangu huu kesho mapema mjisalimishe kwa Mkurugenzi mkitoka na nipate taarifa jinsi walivyoshughulikiwa, hatuwezi kuleana kienyeji lazima tufuate sheria ili tunyooke na kuwatumikia wananchi wetu kwa kutoa huduma bora" Ameongeza RC Sanare.
Mbali na hapo, amekemea vikali kuwepo kwa zamu za kuingia mdarasani kwa yale madarasa yenye mitihani huku akiwataka Waalimu wajipange vizuri kuhakikisha madarasa yote yenye mitihani ikiwamo darasa la Nne na la Saba wanaingia na kukaa madarasani kwa masaa yaliyoelekezwa na Wizara ya Elimu ya saa 11 jioni kama ilivyopangwa.
Katika kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana amehakikisha kwamba anaboresha madarasa ya TRC yaliyopo katika Manispaa ya Morogoro pamoja na kuwakabidhi Darasa la saba Shule ya Msingi Kikundi kiasi cha shilingi 300,000/= kwa ajili ya kununulia vifaa vya kufanyia mitihani.
Hata hivyo amewataka Waratibu elimu Kata , Waalimu kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya wataalmu wa afya katika shule zao wanazozisimamia katika kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Mwisho amesisitizia wazazi kuchangia fedha kwa ajili ya watoto kuweza kupata chakula wanapokuwa shuleni ili waweze kusoma kwa bidii wakiwa wameshiba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bkari Msulwa, amewataka wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze kufaulu mitihani yao.
“Mimi natamani sana matokeo yenu yakitoka nikiangalia Shule hizi ufaulu wa juu, , natamani sana na Mungu awabariki mmpate matokeo mazuri huku mkimtanguliza Mwenyezi Mungu mbele,kikubwa zingatieni masomo na kuwaheshimu Walimu wenu” Amesema DC Msulwa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mnaispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema katika kuhakikisha vituo vya mafunzo vya TRC vinaboreshwa ,atawasilisha taarifa CMT pamoja na kujadilina na idara ya elimu Msingi kuona jinsi watakavyoiweka katika Bajeti fedha za ukarabati wa vituo hivyo kwa ajili ya kunyanyua viwango vya ufaulu na taaluma kwa Shule za Manispaa ya Morogoro.
Miongoni mwa Shule alizotembelea Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ,Mhe. Loata Sanare ni pamoja na Shule ya Msingi Kikundi, Shule ya Msingi Kilakala na Shule ya Msingi Mwande .
Post a Comment