Header Ads

DC MSULWA ATAKA ZOEZI LA UGAWAJI VIZIMBA VYA BIASHARA SOKO KUU LIENDESHWE KWA UTULIVU.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa , akizungumza na Wafanyabiashara Soko la Mawenzi.(kushoto) Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John.

Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John, akifuatilia kwa makini Mkutano huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro  ,Dr Tito Kagize, (katikati),akipitia taarifa katika Mkutano wa Wafanyabiashara Soko la Manzese.

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amelitaka zoezi la ugawaji wa Vizimba vya Wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kisasa Manispaa ya Morogoro lifanyike kwa utulivu na amani.

Kauli hiyo ameitoa jana Julai 23,2020 wakati wa mkutano na Wafanyabiashara wa Soko la Manzese katika kuwapa utaratibu ambao Manispaa ya Morogoro  umeupanga.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Msulwa, amesema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika Soko hilo hivyo itakuwa ni jambo la aibu zoezi hilo kama litatawaliwa na vurugu na fujo.

Msulwa, amesema kabla ya zoezi la kuwaingiza Wafanyabiashara hao Sokoni lazima waanze kutengenezewa namba zao na kuoneshwa maeneo watakayokaa katika vizimba vyao ili wakati wa zoezi kusiwe na fujo wala viashiria vya uonevu.

"Nimesikia kwamba kuna utaratibu wa wafanyabiashara kuingia hapa Sokoni, lakini niwaombe wahusika huu utaratibu ili ufanyike vizuri wachukueni wale ambao wameshakuwa katika vigezo vyenu mkawaoneshe Vizimba vyao kwanza kisha muwape namba zao na wale ambao watakosa sifa muanze utaratibu wa kuwapa hizo fomu bila upendeleo ili hao wenye sifa wakishaingia na hawa wasikose maeneo ya kufanya biashara ili waendelee kutafuta ridhiki zao, itakuwa jambo la aibu zoezi hili likatawalia na vurugu, tutakuwa hatujamtendea haki Mhe. Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli kwa kutupatia heshima kubwa ya mradi huu ambao ndio mkombozi wa Manispaa yetu" Amesema DC Msulwa.

Katika hatua nyingine, Msulwa, amesema Serikali ipo makini  sana na  haitofumbia macho chokochoko zenye viashiria vya uvunjifu wa amani katika Soko hili.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro  ,Dr Tito Kagize,  amesema wamejipanga vizuri katika zoezi la ugawaji wa Vizimba huku akisema ushauri wa Mkuu wa Wilaya wameupokea na kuufanyia kazi kwa ajili ya masilahi ya Serikali na Wafanyabiashara  watakaokuwa wanafanya biashara katika Soko hilo bila upendeleo wowote.



""Tumejipanga vizuri sana, utaratibu wa kuwaorodhesha  wale wafanyabiashara waliosaini mkataba awali kupisha ujenzi wa Soko hili umekamilika mpaka sasa tuna jumla ya wafanyabiashara  764  ambao wanatokea Soko la Mawenzi  na Manzese ambao tuliwaondoa Soko la zamani kupisha ujenzi wa Soko hili na wale wataokosa sifa za kuingia kama ulivyotuelekeza tutaanza haraka zoezi la ugawaji wa fomu na tutalisimamia vizuri kwa umakini bila upendeleo ili nao wawe na sifa za kufanya biashara katika Soko hili"" Amesema  Dr Kagize.

Dr Kagize, amewataka Wafanyabiashara hao wa Manispaa ya Morogoro, kuwa watulivu kwani soko hilo linavyo vizimba vya kutosha.

Kwa upande wa Mweka hazina wa Manispaa ya Morogoro , Ponceano  Kilumbi, amesema mpaka sasa jumla ya wafanyabiashara  764 ndio wamekuwa na sifa za kupata Vizimba  Sokoni hapo, ambapo Soko la Manzese ni wafanyabiashara 446 wamehakikiwa wenyesifa ni 399 wasio nasifa 47 na Soko la Mawenzi waliohakikiwa 398 wenye sifa 365 na wasio na sifa 33.

Kilumbi amesema vizimba vipo 900 wakati  idadi ya wafanyabiashara  wanaotakiwa kupata Vizimba ndani ya soko hilo  ni 764 waliokuwa na wasio na sifa 80 ambapo  hesabu inayoonyesha kuwa vizimba  136   vitabaki bila kutumika.






No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.