Header Ads

DC MSULWA ATAKA VYANZO VYA MAJI VILINDWE KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MAJI.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, akizungumza na Wananchi waliojitokeza kwenye Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi uliofanyika kwenye eneo la shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege leo Julai 16, 2020.



Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,  akizungumza na Wananchi waliojitokeza kwenye Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi uliofanyika kwenye eneo la shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege leo Julai 16, 2020.

Mmoja wa wananchi akitoa kero zake mbele ya Mkuu wa Wilaya.
Jengo jipya la Ofisi ya Kata ya Uwanja wa Taifa.
Jengo jipya la Ofisi ya Kata ya Mindu.

Jengo jipya la Ofisi ya Kata ya Chamwino.


MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amesema vyanzo vya maji ni lazima vilindwe ili kukabiliana na changamoto za usimamizi wa rasilimali za maji kwa sababu kuna uhaba wa rasilimali za maji unaopelekea upatikanaji wa maji kuwa na mapungufu makubwa kulingana na mahitaji.

Kauli hiyo ameitoa leo Julai 16,2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za  Wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwenye eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege Manispaa ya Morogoro ambapo ametembelea Kata tatu (3) zikiwamo Kata ya Chamwino, Mindu pamoja na Uwanja wa Taifa .


Msulwa, amesema hivi sasa kumekuwa na Ongezeko la mahitaji ya matuminzi ya maji kwa ajili ya majumbani, kilimo, viwanda ,  hivyo kila mwananchi anawajibu wa kuvilinda vyanzo vya maji ili kuendelea kupata huduma hiyo bora ambayo imebeba asilimia kubwa ya uhai wa mwanadamu.

“Upatikanaji wa maji ni changamoto kutokana na Ongezeko la watu na upanukaji wa mji katika Manispaa yetu ya Morogoro,  kama nilivyopata kero za maji inaonekana hii ni changamoto kubwa katika maeneo yetu  na tusipo simamia vizuri katika utunzaji wa vyanzo vya maji itafika mahala tunakosa kabisa kwa matumizi, lakini ndugu zetu wa MORUWASA kupitia Mkurugenzi Mtendaji wameshatuelezea mipango yao kikubwa tuwe na subira tuone na sisi kwa upande wetu wa Wilaya tutapitia hiyo mipango ili tuongeze msukumo maji yapatikane na tuondoe kero hii kwa ustawi wa jamii zetu, lakini hatutakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote anaye haribu vyanzo hivi, tutawakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria , tunatakiwa kutumia maji tuliyonayo vizuri” Amesema DC Msulwa.

Aidha, amesema vyanzo vya maji lazima visimamiwe ili kuhakikisha rasilimali hiyo ya maji inapatikana ya kutosha na inakuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo .

Amesema kuwa wananchi wengi hawana uelewa kuhusiana na uhifadhi wa maji na kusababisha vyanzo hivyo kuingiliwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo uvuvi, kilimo pamoja na ufugaji.

“Vyanzo vya maji chanzo kikuu ni mvua, hivyo kila mmoja akivuna maji ya mvua mwisho wa siku maji hayo yanayohifadhiwa chini ya ardhi na kutumika kama vyanzo vya chini na juu ya ardhi yatakosekana” Ameongeza DC Msulwa.

Naye Mkurugenzi wa MORUWASA, Mhandisi Tamimu Katakweba, amesema huduma ya maji ambayo kupitia watoa huduma hiyo hususani mamlaka za maji , yanatokana na uhifadhi unaofanywa na Bodi za maji za Mabonde (ambayo  ni 9) yaliyopo nchini ambapo yanayotekeleza sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji Na. 11 ya mwaka 2009.

“Shughuli za kibinadamu katika ndani ya mita 60 ya vyanzo vya maji zinazuliwa kufanyika na kuwepo kwa shughuli hizo ni kinyume cha sheria ya maji ya usimamizi wa rasilimali za maji pia sheria zinakataza kuvuna maji ya mvua endapo kiwango kitazidi zaidi ya lita 20,000 lazima uvunaji wa maji hayo yapate kibali” Amesema Eng. Tamimu .

Katika hatua nyengine, amesema katika kuhakikisha maji  changamoto ya maji inaondoka washabadili usanifu wa awali uliowekwa mwanzo wa kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 ambao ulikuwa ni mradi wa chini lakini sasa wameweka usanifu mpya ambao mradi wake utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 2.9 na mpaka sasa kiasi cha shilingi milioni 160 zishaingizwa na utekelezaji una muda wa miezi 2 kati ya miezi 14 iliyopangwa ili kukamilisha mradi huo.

Pia amesema wapo katika mkakati wa kupanua  Bwawa la Mindu ili kuongeza wingi wa  maji na kufanya wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuweza  kunufaika zaidi na huduma ya maji .

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.