MKURUGENZI MANISPAA MOROGORO AFUFUA MATUMAINI YA UJENZI WA SHULE MPYA YA MSINGI KATA YA MZINGA.
Wananchi wakinyoosha vidole kuashiria kuridhika na maamuzi ya upatikanaji wa eneo la Ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Kata ya Mzinga. |
Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro Bi Chausiku Masegenya (watatu kutoka kulia) akioneshwa mpaka wa Msitu na Makaburi ambapo kunatarajiwa kujengwa Shule ya Msingi. |
Mwenyekiti wa Mila na Desturi Mkoa wa Morogoro Ramadhani Divu Nyagale akizungumza na Wananchi katika Mkutano.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mzinga , Ndg Erick Mshana, akizungumza na Wananchi.
Wananchi wakipata vinywaji mara baada ya kumalizika kwa Mkutano. |
MKURUGENZI Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba, amemuagiza
Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, kusimamia kikamilifu wananchi wa Kata
ya Mzinga kuunda Kamati ya Ujenzi wa Shule mpya ya Msingi ambapo ilikuwa ni
kero kubwa katika Kata hiyo.
Kauli hiyo ameitoa leo Julai13,2020 kufuatia kumalizika kwa sintofahamu ya juu ya mmiliki aliyedaiwa kumiliki eneo
la Msitu mdogo uliopo Kata ya Mzinga Mtaa wa Kidangawa maarufu kama Kongwa.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema Kata ya
Mzinga ni miongoni mwa Kata 29 zilizopo Manispaa ya Morogoro ambayo haina shule
hata moja huku watoto wakisoma katika Kata jirani ambazo zipo mbali na makazi
yao.
Lukuba, amesema mgogoro huo umemalizika leo muda
na wakati wowote wakazi wa Kata ya Mzinga wajiandae na mradi wa ujenzi wa Shule
mpya ya Misngi ambayo itaingia katika historia yao na kusogeza karibu huduma ya
shule kwa Watoto.
“”Nawashukuru sana Afisa elimu Msingi Manispaa ya Morogoro , Afisa Tarafa
Manispaa ya Morogoro , wataalamu wa Misitu ,Viongozi wa kimila Mkoa na Wilaya,
Viongozi wa Kata, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mzinga pamoja na Wananchi kwa
kukubali kauli moja ya kujenga shule, Kata hii bado ipo nyuma huduma za Shule,
leo tumekubaliana , nimemuagiza Afisa Elimu alisimamie hili ili kamati ya Ujenzi
ianzishwe mara moja na waanze kwa utaratibu wa kuhamasishana wenyewe katika uchangiaji wa fedha za Ujenzi kwa kuwa eneo lipo tayari , na sisi
katika Bajeti yetu ya mwaka wa fedha ujao wa 2021/2022 tuitengee Bajeti ili
watoto wasome karibu na makazi yao” Amesema Lukuba.
Hata hivyo, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya
Morogoro,Bi Chausiku Masegenya, amewashukuru Wananchi kwa kufanya maamuzi yenye tija kwa ajili ya
maendeleo ya Watoto na vizazi vijavyo.
“”Nimekuja kumwakilisha Mkurugenzi, lakini
nimefurahi sana maamuzi haya, nitaongea na Mhandisi wa Manispaa afike katika
eneo hili aangalie eneo kisha awaelekeze jinsi ya kufanya ili wakazi hawa waanze mara moja usafi na waandae kamati za ujenzi na uhamasishaji kwa ajili ya kuchangia fedha, wakionesha nia nzuri sisi katika vikao vyetu vya kibajeti tutawasilisha ili tupate fedha
za kuendelea na ujenzi , ningependa mwakani wanafunzi wasiandikishwe Kauzeni
waandikishwe kwenye Shule yetu mpya najua Mkurugenzi wangu mpambanaji ana amelifufua hili tutafanikiwa kwa asilimia 100 ””Amesema Bi Chausiku.
Kwa upande wa Afisa Tarafa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako , akizungumza kabla ya kumkaribisha Afisa Elimu Msingi kuzungumza na Wananchi hao, amesema
sula la elimu linatakiwa kupewa uzito wa hali ya juu katika kujikomboa na
kujinasau na umasikini.
Kipako, amesema haiwezekani mtu mmoja
akawa juu ya wenzake kwa kupinga maendeleo ya elimu.
Naye aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mzinga, Mhe.
Milikieli Mahiku , amewapongeza Wananchi wa Kata ya Mzinga kwa maamuzi yenye
uthubutu huku akitoa ahadi ya mifuko 30 ya Saruji katika kuchangia Ujenzi wa Shule hiyo ya Msingi .
“Sijatoa ahadi hii kama
kampeni,nimetoa ahadi hii kwa kufurahishwa na maamuzi ya wananchi hawa, ni muda
mrefu suala la shule tulikuwa tunalihitaji lakini leo jambo limekaa mahala pake
lazima nimfurahie zile jitihada ambazo awali tulizitaka zitokee, nieleweke
kwamba sitogombea tena Udiwani, nitaangalia nafasi nyengine zaidi ya kugombea lakini
nitahakikisha nashiriki nao kwa kila jambo wananchi wa Kata hii hata kama
sitakuwa kiongozi bado nitakuwa nao bega kwa bega nikiwa mwananchi wa kawaida”
Amesema Mhe. Milikieli.
Mwenyekiti wa Mila na Desturi Mkoa wa
Morogoro Ramadhani Divu Nyagale ,amesema
mila hazikatazwi lakini lazima kutengwe eneo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa
Shule ambapo mara baada ya kukamilika itawarahisishia wanafunzi kupata elimu
bora pasina mateso wanayoyapata sasa kutokana na ukosefu wa shule ya serikali
ya Msingi na Sekondari katika Kata nzima ya Mzinga.
Naye Shabani Matunda, ambaye ni wakazi wa Mtaa wa Kidangawa Kata ya Mzinga amemuomba Mkurugenzi wa Manispaa kutilia mkazo swala la upatikanaji wa Shule huku akimpongeza Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro Bi. Chausiku Masegenya akimwakilisha Mkurugenzi kwa kuzuru katika eneo hilo lililokuwa na utata kwani ameonyesha uwezo wa kujali wananchi anaowaongoza.
Ili kufanikisha Ujenzi wa Shule hiyo , aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mzinga, Mhe. Mhe. Milikieli Mahiku aliahidi mifuko 30 ya Saruji, Mtendaji wa Kata ya Mzinga Jerry Kiwelo ameahidi mifuko 10, na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mzinga , Ndg Erick Mshana ameahidi mifuko 5 na kufanya jumla ya ahadi kutimia mifuko 45 ya Simenti.
Post a Comment