Header Ads

DC MSULWA AWATAKA WANAMICHEZO KUZINGATIA NIDHAMU

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa (katikati) akifurahi na kuonyesha Jezi aliyozawadiwa  na Mkurugenzi wa Fountain Gate Sports Academy baada ya uzinduzi wa Kituo hicho. (kushoto ) Mkurugenzi wa Fountain Gate  Sports Academy , Japhet Makau (kulia ) Kaimu Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Jimmy Katabaruki.



Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa akizindua Kituo  cha Fountain Gate Sports Academy.(katikati)Mjumbe wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA)  Ndg. Alex Bulenga .

Kaimu Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Jimmy Katabaruki akitambulisha Viongozi wa ngazi ya Wilaya ya Morogoro.

Mkurugenzi wa Fountain Gate  Sports Academy , Japhet Makau, akizungumza mara baada ya uzinduzi wa Kituo hicho.
Mohamed Muya, Kocha Mkuu wa Fountain Gate Sports Academy.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, akizungumza na Vijana kabla ya mchezo ulioandaliwa kwa ajili ya uzinduzi wa Kituo hicho kuanza.
Kikosi cha Fountain Gate Sports Academy chini ya Umri wa miaka 15.
Kikosi cha  Tanzanite Sports  Academy chini ya Umri wa miaka 15.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa,(watatu kutoka kushoto)  akiwa na Uongozi wa Fountain Gate Sports Academy , Kaimu Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro (wapili kutoka kushoto)  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Boma A Kata ya Mazimbu (kushoto)  Mhe. Kilewa Bohari wakifuatilia mtanange wa Vijana hao.

MKUU  wa Wilaya ya Morogoro,Mhe. Bakari Msulwa,  amewataka wanamichezo  nchini kuzingatia nidhamu na uvumilivu ili kufikia malengo yao.
Hayo ameyasema leo Julai 25,2020 wakati akizindua Kituo cha kukuzia na kulea Watoto cha Michezo cha Fountain Gate  Sports Academy, kilichopo Mtaa wa Boma A Kata ya Mazimbu Manispaa ya Morogoro.
Katika Uzinduzi huo, Msulwa, amevitaka Vituo vya Mafunzo kwa Watoto wanaolelewa katika tasinia  ya michezo kuwa na utayari wa kuwafundisha nidhamu pamoja na   kujifunza mbinu mbalimbali za  kuendeleza na kukuza vipaji vya wachezaji wao.
“Akademiki  hizi ni muhimu na elimu tosha kwa vilabu vyetu nchini katika kuhakikisha vipaji vya wanamichezo vinakuzwa na kuendelezwa ili kufanikisha maendeleo ya sekta ya michezo, hivyo tukiwalea Watoto hawa katika nyanja ya nidhamu ya hali ya juu tutakuwa tunatengeneza Taifa la Wachezaji wanaojitambua na kuthamini Vipaji vyao  na kuletea Taifa heshima katika tasnia ya michezo hapa nchini  “Amesema DC Msulwa.

Msulwa, amesema  mbali na  nidhamu lakini pia Vituo  hivyo vinatakiwa kuweka misingi  ya usimamizi mzuri wa Watoto juu ya taaluma shuleni ikiwemo kuweka utaribu wa kujisomea mara watokapo mazoezini .
""Michezo sio afya pekee, zamani michezo ilikuwa ni ridhaa, sasa hivi ni ajira unawaona wakina Samata na Msuva wote walijiwekeza katika nidhamu , malengo wakafanikiwa lakini lazima wachezaji wetu wawe na njia mbadala ikiwemo elimu kwani ni njia rahisi ya wao kufundishika zaidi na kufikia malengo waliyojiwekea, tuwafundishe mpira, nidhamu na tuwape fursa ya wao kusoma zaidi nakushukuru Mkurugenzi wa Fountain Gate Sports Academy kwa hatua uliyofikia ambapo kuna kila sababu Serikali kukuunga mkono kwa vile unafanya kitu kizuri chenye kuzalisha ajira kwa Watoto wetu " Ameongeza DC Msulwa.
Baada ya uzinduzi wa Kituo hicho, DC Msulwa, alipata muda  kufungua mchezo wa ufunguzi wa Kituo hicho ulioandaliwa kati ya Vijana wa Fountain Gate Sports Academy dhidi ya Vijana wa Kituo cha Akademiki cha Tanzanite.
Amesema upo mpango amabo anausuka wa kuhakikisha anafufua michezo Wilaya ya Morogoro kwa kuwakutanisha Wanamichezo mbalimbali ikiwemo Taasisi za Serikali na Binafsi kukutana eneo moja kwa ajili ya kuzungumza michezo kwa pamoja.
""Kuna mpango na usuka, nitamshirikisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Ofisi za Wakurugenzi , Vyama vya Soka, Taasisi binafsi pamoja na wadau wa michezo ili tutenge siku ya pamoja ambayo tutaiita siku ya Wanamichezo lengo tuzungumze kwa sauti moja na kufufua michezo na kurudisha heshima ya Morogoro katika michezo, maana tukiwa kimya sana tunasababisha hata viwanja vyetu kuwavimiwa na wananchi na watoto wetu wanakosa mahala pa kufanyia michezo, lakini hata ile migogoro ya kijamii tukikutana pamoja tunaweza kuimaliza au kuipunguza "Ameongeza DC Msulwa.
Kwa upande wa Kaimu Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Jimmy Katabaruki, amewataka wamiliki wa Vituo vya michezo waendelee kuwa na moyo wa kuwalea Watoto lakini kubwa kuwafundisha  jinsi ya kuwa na hofu ya Mungu katika kulea vipaji vyao.
Amesema mipra ya siku hizi kuanzia mitaani hadi timu kubwa zimekuwa zikiingia katika imani potofu sana jambo ambalo linashindwa kufikisha gurudumu hili la michezo mbele.
""Hawa watoto ukishawajenga katika imani hizo za kishirikina , unawatoa mchezoni kwani wanaamini kwamba watapata matokeo mazuri na kuacha ile nguvu ya ushindi yenye kutumia vipaji walivyopewa na Mwenyezi Mungu kutoitumia, ni vyema dhana hiyo ikatolewa na ikiwezekana baada ya mazoezi watafutwe waalimu wa kiimani wawafundishe juu ya kuwa na hofu na Mungu ili vipaji walivyopewa wavitumie vizuri kuwaletea matokeo chanya"Ameongeza Katabaruki.
Katabaruki ,amesema michezo ni ajira hivyo kila mwanamichezo aelekeze nguvu yake huko huku akizingatia nidhamu, elimu, utiifu na kuwa na hofu ya Mungu ili kuendelea kulinda Vipaji vyao.
"Zamani tulikuwa tunajua michezo watu wanafanya baada ya kuchoka kufanya shughuli fulani, hata Shuleni ratiba ya michezo kwa wanafunzi inafuata baada ya wanafunzi kuchoka kusoma  lakini kupitia Akademic hizi watoto wanapata maarifa, ufafanuzi na kushirikisha Vipaji vya mtoto katika kuinua hatima ya maisha yake, nawapongeza sana wadau wa michezo kwa uwekezaji huu naimani miaka ya mbele Wilaya yetu ya Morogoro hususani manispaa yetu ya Morogoro  itakuwa na wanamichezo maarufu na wenye majina makubwa kupitia vituo hivi vya mpira" Amesema Katabaruki.

Naye Mkurugenzi wa Fountain Gate  Sports Academy , Japhet Makau, kuwa lengo kuu la kujenga Vituo hivyo vya michezo  kwa Vijana wa Tanzania  ni kujenga uhusiano mzuri katika michezo hususani mpira wa miguu kwa kuweka msingi mzuri wa kusaidia klabu za michezo na kukuza vipaji kwa vijana.
Makau, amesema kuwa adhima yao kubwa ni kuhakikisha kuwa wanawapa nafasi Vijana ya kuonesha Vipaji vyao na kuwakuza katika michezo.
"Sisi tunaamini mpira ni ajira kubwa, kinachotakiwa ni Vijana kutayarishwa, kuendelezwa  na kuweza kupata mafanikio makubwa timu yetu ya Fountain Gate Sports Academy ya wakubwa tumepata nafasi ya kwanza Ligi Daraja la Pili na kufanikiwa kuingia Ligi Daraja la kwanza haya ni mafanikio makubwa ya uwekezaji kwa Vijana , zamani tulikuwa tunasikia lakini sasa tumeona na kushuhudia watu kama Mbwana Samata , Saimoni Msuva wakipata fedha nyingi kupitia mpira, naamini tukiwaandaa vijana wetu hawa watakuwa vijana wazuri na kucheza mpira Tanzania na nje ya nchi na kuwapa ajira mbadala badala ya kutegemea elimu peke yake" Amesema Mkau.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.