Header Ads

WENYEVITI WA KAMATI NA WAWAKILISHI WA SHULE ZA MSINGI MANISPAA YA MOROGORO WAKUTANA NA UONGOZI WA MANISPAA KUJADILI MWENENDO WA UTOAJI WA TAALUMA NA CHANGAMOTO ZAKE


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga , (katikati), akifungua mkutano wa wadau wa elimu. kutoka kulia Afisa Elimu msingi Abdul Buhety, Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Michael Waluse (anayemfuatia Meya) pamoja na Afisa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Bigambo Thomas.
Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Michael Waluse, akizungumza na wadau wa elimu katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilakala.

Afisa Elimu msingi Abdul Buhety, akitoa taarifa juu ya hali ya mwenendo wa Taaluma katika Shule za Msingi Manispaa ya Morogoro.
Afisa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Bigambo Thomas, akitoa maelekezo kwa wadau wa elimu Shule za Msingi.

Wadau wa Elimu , Wawakilishi wa Wazazi mitihani ya darasa la saba na la nne pamoja na Wenyeviti wa Kamati za Shule za Msingi Manispaa ya Morogoro wakiwa katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilakala.









WENYEVITI pamoja na wawakilishi wa  Kamati  za Shule za Msingi za Serikali Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wamekutana na Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kujadili mwenendo wa utoaji wa Taaluma na changamoto zake.
Akizungumza na Waandishi wa habari mgeni rasmi katika mkutano huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, amesema majadiliano yatokanayo na kikao ndio yatakuwa maamuzi ya moja kwa moja kwa ajili ya maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Morogoro.
Kihanga, amesema Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ilikuwa kinara  kwa miaka yote katika matokeo ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi lakini ilipofika mwaka 2017 hali ya matokeo ilianza kubadilika kwa kuwa nyuma ya Halmashauri za Ulanga na Malinyi.
Amesema kuwa ufaulu ulikuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka isipokuwa mwaka 2019 ulishuka kutoka asilimia 88.13 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 87.74 mwaka 2019.
Aidha, amesema miongoni mwa sababu zilizosababisha  kushuka kwa ufaulu ni pamoja na Ongezeko kubwa la uandikishaji wa Wanafunzi kufuatia utekelezaji wa dhana ya Elimu  bila malipo  ambapo ongezeko hilo halijaenda sambamba na idadi ya miundombinu ya madarasa iliyopo pamoja na kukosekana mitihani ya mara kwa mara ya majaribio ambapo hapo awali ilikuwa ikidhaminiwa na michango ya wazazi kabla ya kuanza kwa elimu msingi bila malipo.
Amesema kwa sasa mahitaji ni vyumba 1,556 vya madarasa wakati vilivyopo ni 658 na kufanya kuwa na upungufu wa vyumba 898 vya madarasa hali ambayo ilisababisha shule nyingi za msingi kusoma kwa zamu mbili kwa siku (Double Sessions) ambapo utaratibu huo unaathari kama vile wanafunzi kujifunza kwa masaa 5 kwa siku badala ya masaa 8 kwa kuwa baadhi ya vipindi haviingii kwenye ratiba kuu ya masomo, pia ukubwa wa madarasa huwafanya walimu kushindwa kufundisha kwa ufanisi (Un manageable classes) pamoja na kuchochea utoro hasa wanafunzi wa zamu ya mchana kwa kuchelewa kufika nyumbani usiku.
Kuhusu michango, amesema tangu kutangazwa kwa Elimu msingi Bila malipo, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ikipeleka fedha kila mwezi kupitia akaunti za shule za msingi kwa ajili ya kugharamia elimu kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanyonge.
"Serikali imekuwa na dhamira ya dhati sana ya kuwasaidia wananchi wanyonge katika kukuza elimu nchini lakini kutokana na ukubwa wa Sekta ya Elimu bado kumekuwa na changamoto nyingi zinazozikabili shule za msingi hapa nchini zikiwemo kiasi cha fedha kinachopokelewa na shule ni kidogo ukilinganisha na gharama halisi za uendeshaji wa shule, fedha zinazopokelewa kuwa na mchanganuo maalum wa matumizi na hivyo matumizi mengine nje ya yale yaliyoainishwa husababisha hoja za ukaguzi pamoja na fedha hizo hazijumuishi gharama za malipo ya Ankara za Maji, Umeme na malipo ya Walinzi wa shule na hivyo kupelekea shule zote kukatiwa maji na kuibiwa kwa vifaa mbalimbali kwa kukosekana kwa ulinzi"Amesema Mh. Kihanga.
Akifafanua zaidi Mhe. Kihanga, amesema Serikali  kwa kuzitambua changamoto hizi, ilitoa mwongozo uliowataka Wazazi, jamii na Wadau kuchangia katika kutatua kero zinazozikabili shule za msingi ambapo katika Manispaa ya Morogoro utaratibu huo ulikumbwa na changamoto.
Miongoni mwa chanagmoto hizo ni pamoja na Wananchi walio wengi wameelewa vibaya tamko la Elimu msingi bila malipo, na hivyo kutokuwa tayari kuchangia chochote , hata kwa mambo ya msingi kwa manufaa ya Watoto wao kwa kisingizio cha Elimu bila malipo pamoja na tabia ya kuwashtaki Walimu Wakuu katika mamlaka mbalimbali kwa mambo waliyokubaliana wenyewe katika vikao halali.
Katika hatua nyingine , Meya Kihanga ameshauri kuwepo na Kambi maalum ya wanafunzi wanaofanya mitihani Darasa la nne na la saba angalau kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya mitihani yao ya Taifa ili kuweka mazingira mazuri ya ufaulu na kuwaweka watoto katika uangalizi mmoja uku akiamini njia hiyo itasaidia sana kupata matokeo chanya na kurudi katika nafasi walizokuwa wakishikilia mwanzoni.
Pia amesema vikao hivyo vya kujadili maendeleo ya elimu wameanza na wadau wa elimu na Kamati za Shule za msingi lakini baadae watakwenda kumalizia na wadau wa elimu na kamati za shule za Sekondari.
Hata hivyo Mhe. Kihanga, aliwataka wazazi mara baada ya kupata kibali kamati zifungue akaunti za benki ili pesa zikae huko na zisikae katika mikono ya watu ili kuleta usalama na uaminifu.
Mwisho amesema anaimani kwamba kikao cha Wadau wa elimu , Kamati za Shule kitakwenda kuwapatia mikakati itakayoinua kiwango cha taaluma cha watoto wa Manispaa ya Morogoro na kuondokana na aibu ya kuzidiwa kitaaluma na Halmashauri za pembezoni zenye changamoto nyingi na kikao hicho kitaibua suluhu ya changamoto zinazozikabili shule za msingi zilizopo Manispaa ya Morogoro ikiwemo ukosefu wa Chakula kwa Watoto , kukatwa kwa maji na kuibwa kwa mali za shule.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse, amesema yale yote waliyoyajadili katika kikao hicho watakwenda kuyafanyia kazi.
Amesema lengo la kukutana ni kuona ni kwa namna gani Kamati za shule zinakwenda kushirikiana na waalimu na wazazi  ili kuboresha na kuinua viwango vya ufaulu na kupata matokeo chanya katika Manispa ya Morogoro.
"Tuanze hapa tulipo kama wenzetu wameweza sisi tunashindwaje? nafikiri hiki ni kikao halali cha maamuzi ya pamoja , haiwezekanai Manispaa yetu tushike nafasi ya tatu tushindwe na Halmashauri za pembezoni ambazo zina chanagmoto nyingi, tubadilike sasa tuendelee kushikamana na nyie mliokuja leo muwe mabalozi wa kusambaza taarifa hizi kwa wenzenu ili tupige hatua matokeo hayaridhishi tukibwetea sana tutaikosa hata hiyo nafasi ya tatu tutazidi kushuka jambo ambalo litakauwa ni aibu kwa sisi tulio mjini " Amesema Waluse
Naye Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro Abdul Buhety amesema kitendo cha wanafunzi kutoka saa 9 mchana kinapelekea wanafunzi wengi kutorudi nyumbani na matokeo yake wanaishia kati kati na kufanya mambo ya ajabu.
Amesema wamechukua jitihada nyingi sana za kuhakikisha ufaulu unaongezeka lakini wapo watu wachache  ambao ni waharibifu lakini watashughulikiwa ili maendeleo ya Elimu katika Manispaa ya Morogoro yaongezeke.
"Sina hakika sana hawa wanaowashtaki walimu wakuu ni wazazi au la pengine inawezekana watoto zao wanasoma shule za kulipia au watoto wao hawana akili sasa wanataka kuwaambukiza watoto wengine, niwaombe ndugu zangu tuwekeze katika elimu tusipokubali kubadilika sisi wazazi hata watoto wetu hawawezi kubadilika, kitendo cha  kuwastaki walimu kwa vikao halali mlivyokubaliana  sio jembo jema" Amesema Buhety.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.