Header Ads

DC CHONJO AGAWA HATI MILIKI ZA KIMILA 159 KWA WANANCHI WA KIJIJI CHA MIKESE HALMASHAURI YA WILAYA YA MOROGORO.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo akitoa hati kwa mmoja ya mwananchi wa kijiji cha Mikese Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Frolence Mwambene akifafanua jambo wakati wa zoezi la ugawaji wa Hatimiliki ardhi za Kimila.

wananchi wa kijiji cha Mikese waliohudhulia mkutano wa kutoa hati miliki.

Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Bi:Ruth John,  akizungumza na kutambulisha wageni kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya  kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya kendelea na mkutano wa ugawaji Hatimiliki ardhi za Kimila.


MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ametoa hatimiliki za Kimila 159  kwa Wananchi wa Kijiji cha Mikese kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Tukio hilo la ugawaji wa hatimiliki za ardhi za kimila limefanyika leo Februari 24, 2020 katika viwanja vya Shule ya Msingi Mikese likiwa na lengo la Wananchi kumiliki ardhi watakayoitumia kwa maendeleo yao endelevu katika jamii. 

Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Chonjo, amesema,hati hizo zimetolewa na kufadhiliwa na Taasisi zisizo za Kiserikali ikiwamo Shirika la kuhifadhi Misitu  Tanzania   (TFCG) chini ya Mradi wa Mkaa Endelevu;Haki Ardhi, PELUM Tanzania na Morogoro Paralegal.

“Leo tumeshuhudia tukifanya tukio la ugawaji wa Hatimiliki za ardhi za  Kimila 159 katika Kijiji chetu cha Mikese, hatutarajii kusikia ugomvi tena utokee, nitoe angalizo wapo Vijana wanawasubiria wazazi wao wapate hati ili waziibe na kwenda kuzigeuza fedha, lindeni na mzitunze vizuri na muone kama nidhahabu kwenu,msiziweke hovyo , kuna michezo michafu tusimuamnini kila mtu, tumefanya jambo jema leo sasa kesho lisejeleta adha kwangu na kwa vyombo vya sheria" Amesema DC Chonjo.

DC Chonjo, amesema kuwa , ugawaji wa Hatimiliki za kimila kwa Kijiji cha Mikese ulipangwa kufanyika wakati wa mbio za Mwenge 2019 lakini zoezi hilo lilisitishwa kutokana na mapungufu yaliyojitokeza na sasa mapungufu hayo yamerekebishwa.

 Aidha, ametoa rai kwa Benki pamoja na vyombo vinavyohusika na utoaji wa mikopo kwamba wanapokuja watu kuomba mikopo na hati za familia wasiwahudumie hata kama barua zao zina mihuli ya Watendaji na Wenyeviti wa Mitaa kwani ipo mihuli feki na wanatakiwa kuwa makini kuepuka kusababisha migogoro katika familia.

Amesema malengo makuu ya kupima mashamba na kutoa hatimiliki za kimila kwa wananchi ni pamoja na kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi kisheria, kuwawezesha wananchi kutumia hatimiliki za ardhi yao kama dhamana ya kukopa katika Taasisi za fedha na hivyo kuinua kipato, kupunguza migogoro ya ardhi na kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Chama Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 inayolenga kuwapatia wananchi Hatimiliki 2,500,000 kwa nchi nzima.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Frolence Mwambene, amesema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa kwani kupitia mradi huo migogoro mingi ya ardhi katika Kijiji husika imetatuliwa ikiwemo migogoro ya mipaka ya Vijiji na kufanikiwa kupima Mashamba 720 kwa ajili ya kuandaliwa Hatimiliki za kimila .

Amesema katika Kijiji cha Mikese peke yake , jumla ya Mashamba  250 yamepimwa na kuandaliwa Hatimiliki za kimila 159 ambazo ziko tayari kukabidhiwa kwa Wananchi leo na hati 91 zilizobaki zina mapungufu na zitatolewa kwa wananchi mara tu baada ya kuondoa mapungufu hayo.

Kwa upande wa Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Patrick Mwakilili,amesema kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na upimaji ardhi una manufaa makubwa katika kupunguza umasikini na njaa katika jamii hasa za vijijini.

Amesema kuwa kila mwananchi katika Halmashauri hiyo anahaki ya  haki ya kupata, kutumia, kumiliki na kugaiwa ardhi ili mradi wafuate sheria na taratibu zilizowekwa.

Aidha, amesema  kupitia mradi huo  jamii  imepata uelewa katika kumiliki ardhi umeongezeka na umesaidia kuwahamasisha kutumia nafasi waliyopewa kuomba ardhi ambayo ni rasilimali muhimu katika kukuza kipato chao.

Katika kijiji hicho amesema kuwa , mradi uliwezesha uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi na  kutoa mafunzo juu ya haki za ardhi na matumizi ya rasilimali ardhi kiuzalishaji ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Amesema , waliopata hatimiliki za kimila wanaweza pia kuzitumia kama dhamana mahakamani na katika taasisi za fedha kupata mikopo itakayowawezesha kushughulikia changamoto walizonazo.

Amesema  jumla ya vijiji 151  kati ya vijiji 132  vya Halmashauri wilaya hiyo vimenufaika na mradi huo ambapo katika kipindi cha Julai 2019 hadi sasa , Halmashauri imeandaa hatimiliki za kimila 452, ambapo  hati 220 kati ya hizo zimetolewa katika Vijiji vya Matuli na Lulongwe na hatimiliki 232 zimetolewa katika Vijiji vya Mlilingwa na Tununguo.

Mwisho amewaomba Wadau hao wa maendeleo waendelee kuwasaidia katika kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji ambavyo bado havina mipango hiyo.

Mmoja wa Wananchi waliopatiwa hatimiliki ya ardhi ya kimila leo , Asha Saidi, amewashukuru Viongozi wa Kijiji, Halmashauri na Mkuu wa Wilaya kwa kitendo cha kuwagawia hati hizo na kusema itamsaidia  kutafuta mikopo atakayoitumia kuwekeza katika shughuli zake za kueleta maendelo.

Ikumbukwe kwamba Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya PELUM ilianza kutekeleza mradi wa upimaji na Urasimishaji wa Ardhi tarehe 10, Disemba 2013 hadi tarehe 9 Juni 2018 katika Vijiji vya Mikese , Mfumbwe, Newland na Lubungo ambapo Mradi huo ulihusisha uandaaji wa Mipango ya matumizi bora ya ardhi, kutoa elimu ya ardhi, kupima vipande vya ardhi/Mashamba na kutoa Hatimiliki kwa wananchi kwa gharama zaidi ya Shilingi Milioni 100 ambapo kuna wananchi mmoja mmoja ambao waligharamia upimaji wa Mashamba yao na kuandaliwa Hatimiliki kwa gharama ya Shilingi 75,000/= kwa shamba moja.







No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.