DC Chonjo atatua kero ya ukosefu wa Ofisi ya Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, akitoa hotuba mbele ya Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro leo. |
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, akihutubia Baraza la Wazee la Manispaa ya Morogoro leo. |
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Bi.Enedy Mwanakatwe akiwa katika Mkutano wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro leo.(kushoto) Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John. |
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro, Ally Rashidi Zongo. |
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr Ikaji Rashid akizungumza jambo katika kikao cha Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro leo. |
Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro, Sidina Mathias (kushoto) akiwa pamoja na Mratibu wa Wazee Manispaa ya Morogoro, Rehema Malimi wakifuatilia kikao cha Baraza la Wazee leo. |
MKUU wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Regina Chonjo, ametatua kero ya muda mrefu ya kutokuwa na Ofisi kwa Baraza la Wazee Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro baada ya leo kuwatafutia Ofisi kutoka Shirika la Nyumba NHC .
Hatua hiyo ameichukua leo kufuatia kikao cha Baraza la Wazee wa Manispaa ya Morogoro kutaka kuonana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kwa ajili ya kumueleza kero na changamoto zao zinazowakabili Wazee hao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, amesema tayari ameshawasiliana na Meneja wa NHC na kukubaliana bei ya pango la kodi ya Ofisi hiyo kuwa Shilingi 70,800/= kwa mwezi.
Aidha, ameahidi kuwapatia Baraza la Wazee kiasi cha Shilingi 500,000/= kwa ajili ya thamani za Ofisi.
DC Chonjo, amesema kuwa wazee ni hazina inayotakiwa kutunzwa ipasavyo kwakuwa ni chachu ya maendeleo ya nchi jambo ambalo hata serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli imekuwa mstari wa mbele kujali afya zao.
Amefafanua kuwa serikali ya awamu ya tano, inawajali wazee na makundi yote ya kila rika, na kwamba kuna haja ya kutoa elimu kuhusu matumizi ya kadi ya afya kwa wazee na hivyo kutoa jukumu hilo kwa wajumbe wa baraza hilo.
Katika hatua nyingine , DC Chonjo, ameipongeza idara ya afya kwa kazi kubwa walioifanya ya kuendesha zoezi la utoaji huduma kwa wazee katika Vituo vinne vya afya vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro huku akisema kuwa huduma hiyo itawasaidia Wazee kwa asilimia kubwa.
"Wazee ni hazina ya Taifa, hivyo yapaswa kupaza sauti juu ya maswala yanayowahusu na kuwasemea haki zao za Msingi pale inapobidi ili waweze kutatuliwa, leo tumekutana na amini kero zenu zile ambazo zipo ndani ya uwezo wangu nitazitatua leo na zile zinazohitaji kupata ufafanuzi wa kina kwa ajili ya kutolea ufafanuzi na maamuzi nitayafanyia kazi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Mganga mkuu pamoja na wataalamu wa idara ili tuone ni kwa namna gani tunaweza kuyafanikisha na kuleta maendeleo chanya kwa wazee wetu" Amesema DC Chonjo.
Hata hivyo, DC Chonjo alipendekeza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kuwachagua baadhi ya wajumbe watatu (3) wa Baraza la Wazee kwa ajili ya kuwakilisha katika Vikao vya Kamati ya Ushauri ya Wilaya ambapo miongoni mwao ni pamoja na Dr Aslam Kidunda, Beatrice Mwogela na Amina Mamuya.
Pia amewataka Wajumbe waliochaguliwa kuingia katika Vikao vya Kamati ya Ushauri kuhakikisha wanakwenda kuwasemea wenzao na kuzifikisha changamoto ili ziweze kutatuliwa.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Bi.Enedy Mwanakatwe, amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuhudhuria katika Baraza hilo la wazee na kutoa ushauri pamoja na mapendekezo juu ya nini kifanyike ili kupelekea gurudumu mbele la Wazee katika Manispaa ya Morogoro.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr Ikaji Rashid, ameainisha mikakati iliyopo ya kuinua hali ya wazee katika Manispaa hiyo kuwa ni kuhakikisha wote wanapata kadi za matibabu, kuwaongezea na kuwajengea uwezo wa kujikwamua kiuchumi pamoja na kuwaunganisha na wadau mbalimbali kwa ajili ya misaada.
Awali akitaja majukumu ya baraza hilo la wazee la Manispaa ya Morogoro, Bi. Sidina Mathias, ambaye pia ni mkuu wa Kitengo cha ustawi wa jamii Manispaa ya Morogoro, amesema Baraza lina majukumu yake ya msingi ambayo ni kupitia majumuisho ya kero za wazee zilizoletwa na wawakilishi, kufanya mkutano wa baraza la wazee la Manispaa kuwasilisha kero za wazee kwenye baraza la madiwani, kuchagua wawakilishi wawili kwenye baraza la madiwani, kushawishi Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya miradi ya uzalishaji ya wazee pamoja na kuratibu mabaraza ya wazee ya Kata.
Naye mratibu wa wazee Manispaa ya Morogoro, Bi. Rhema Malimi,alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya wazee Manispaa ya Morogoro, amesema ni ya kiridhisha kwani wameweza kuunganishwa kwenye huduma za afya kwa kutengenezewa vitambulisho takribani 4002 vya msamaha wa matibabu kwa wazee .
Katika Hatua nyengine, Baraza hilo limechagua wawakilishi watatu (3) watakaoingia katika Vikao vya Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DDC), ambapo miongoni mwao ni pamoja na Dr Aslam Kidunda, Beatrice Mwogela na Amina Mamuya.
Post a Comment