Header Ads

Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro lapitisha Bajeti ya Bilioni 75,372,267,796.32/= kwa mwaka wa fedha 2020/2021


Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,  akimkaribisha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, kwa ajili ya kufungua mkutano wa Baraza la Madiwani  na    kusoma hotuba ya kuwasilisha rasmi Bajeti ya mwaka 2020/2021 katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa leo Februari 12, 2020.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni  Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga akitoa hotuba katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani (Bajeti)  la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro .




Naibu Meya Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege,Mhe. Sengo Isihaka akiwa katika mkutano wa  Baraza la madiwani (Bajeti).  


Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Komanya Spear Aman, (kushoto), akiwa pamoja na  Diwani wa Kata ya Mwembesongo , Mhe. Ally Kalungwana (katikati)  na Mbunge Viti Maalum, Mhe. Christine Gabriel Ishengoma wakifuatilia kwa makini mkutano wa Baraza la Madiwani (Bajeti). 
Baadhi ya Madiwani wakifuatilia kwa umakini hotuba ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga katika Baraza la Madiwani (Bajeti).



Waheshimiwa Madiwani wakishauriana jambo katika Mkutano wa Baraza la Madiwani (Bajeti). 
Baadhi ya Watendaji wa Kata pamoja  na wageni  wakifuatilia kwa umakini hotuba ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga katika Mkutano wa Baraza la Madiwani (Bajeti). 



Mbunge Viti Maalum, Mhe. Christine Gabriel Ishengoma, akitoa pongezi kwa Manispaa ya Morogoro kutokana na Bajeti nzuri   ambayo watakwenda kuipitia Bungeni.(kushoto) Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Komanya Spear Aman, (katikati), Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana. 
Mchumi Rubeni Urasa (kushoto) , akiwasilisha mapitio ya Bajeti ya mwaka 2019/2020 na mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2020/2021 katika kikao cha Baraza la Madiwani (Bajeti).


Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, katika Mkutano wake maalumu wa Baraza leo Februari 17,2020 , limejadili na kuidhinisha kwa kauli moja bajeti yake ya Tshs  75,372,267,796.32/= kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri inakisia kukusanya kiasi cha Tshs 8,478,799,224.32 ambapo Tsh 498,870,893.41 ni uchangiaji wa huduma za afya na Tshs 271,759,000.00 ni uchangiaji wa ada za wanafunzi kutoka katika vyanzo vya ndani na kiasi hicho ni ongezeko la Tsh 1,772,873,011.45 ambayo ni sawa na asilimia 26.43 ya makadirio ya mwaka 2019/2020 ya Tshs 6,705,926,212.87.

Aidha, amesema kuwa  katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri inatarajia kupokea  kiasi cha Tsh 7,483,018,572 kutoka Serikali kuu na wahisani mbalimbali kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambapo Serikali kuu wanatarajia kuchangia kiasi cha Tsh 5,832,810,000 na Tsh 1,650,208,572 ikiwa ni fedha za nje.
Pia ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri inatarajia kutumia kiasi cha Tsh 59,410,450,000.00 kutoka Serikali kuu kwaajili ya matumizi ya kawaida ya mishahara na matumizi mengineyo ambapo matumizi kwaajili ya matumizi mengineyo yanakisiwa kuwa Tsh 2,495,867,000.00 na itapokea kiasi cha Tsh 2,495,867,000.00 ikiwa ni ruzuku ya matumizi ya kawaida na kati ya hizo Tsh 89,196,000.00 ni fidia ya vyanzo vilivyofutwa.
Akiendelea kuwasilisha mapendekezo ya bajeti, Mstahiki Meya, ameelezea mikakati iliyowekwa ya  kuhakiksha mapato yanakusanywa katika mwaka ujao wa fedha ni pamoja na kupitia upya mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa mapato kwa kuboresha maeneo ambayo yana mapungufu,kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kukusanya mapato,kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini mianya inayovujisha mapato,kupitia upya sheria ndogo za mapato na kutumia mifumo ya ki-electronic katika vyanzo vyote vya mapato.


Amesema kuwa ili kuboresha maisha ya wakazi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Morogoro,  Manispaa imeandaa mpango wa mwaka 2020/2021 na mpango wa muda wa kati 2020/2021 – 2022/2023 unaolenga kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kufikia maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi,na kimazingira kwa wananchi wake.
Meya Kihanga, ametanabaisha kuwa Ili kutekeleza dhana nzima ya ugatuaji wa madaraka , mpango huo umeshirikisha jamii katika mpango shirikishi kuanzia ngazi ya Mtaa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji halisi ya Wananchi katika maeneo yao na kujielekeza katika kutoa kipaumbele maeneo yanayoweza kutoa matokeo ya haraka yatakayosaidia ukuaji wa uchumi kwa haraka na kwa kipindi kifupi.

Ameyataja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuwekeza katika miradi mikubwa ya Kimkakati, kuboresha miundombinu ya Afya, na Elimu,kuboresha hifadhi ya mazingira na ukusanyaji wa taka, kuimarisha ushirikishaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na uboreshaji wa mazingira ya wafanyabiashara wadogowadogo kwa kuwajengea masoko katika maeneo mbalimbali.

Ili kufikia malengo yaliyokusudiwa, Mstahiki Meya amewataka viongozi na watendaji wote kusimamia uimarishaji wa mahusiano mazuri kati ya Serikali ,Mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine, kujenga uwezo na ujuzi kwa watumishi katika utoaji wa huduma, kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na uwazi sambamba na kujenga uwezo kwa viongozi wakiwemo waheshimiwa madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa katika kusimamia shughuli za Wananchi.

Katika hatua nyengine amesema makusanyo ya mapato yameongezeka kwa asilimia 26% kutoka Bilioni 6.7 hadi kufika Bilioni 8.4 kwa mwaka sawa na ongezeko la Bilioni 1.7, jambo ambalo linaonesha njia salama ya Morogoro kuwa Jiji kwani sifa ya jiji inachangiwa na ongezeko la makusanyo.

Mstahiki meya wa Manispaa amesema suala la Stendi ya Msamvu kurudishwa katika mikono ya Manispaa linakwenda vizuri na wanatarajia kukusanya mapato mengi kupitia kitega uchumi hicho ili Halmashauri iendelee kukusanya na hatimaye kuweza kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewashukuru wadau wote waliofanikisha bajeti hiyo zikiwemo kamati zote za kudumu za Manispaa, Serikali kuu iliyotenga kiasi kikubwa .

Amesema kuwa, Miradi iliyotengewa fedha kwa Mapato ya ndani ya Manispaa katika mwaka wa fedha 2020/2021 ni pamoja na ujenzi wa Soko kuu la Kisasa ambapo kiasi cha shilingi 10,059,652,000.00 kutoka Serikali kuu na Tshs 7,596,186,405.00 ni mkopo kutoka Benki Kuu  ya Dunia kupitia mradi wa Uboreshaji wa Miji (ULGSP ) na kufanya gharama za mradi kuwa Tshs Bilinioni 17,655,838,405.65,Ujenzi i wa Stendi ya kisasa ya Daladala Mafiga mkopo kutoka Benki Kuu  ya Dunia kupitia mradi wa Uboreshaji wa Miji (ULGSP ) kwa gaharama ya Tshs Bilioni 5, 247,385,940.49 ambao umefikia asilimia 71,ujenzi wa standi ya Kaloleni yenye gharama ya Milioni 724,762,500.00 hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 15% na mkandarasi amelipwa Tshs 108,714,375.00, pamoja na Ujenzi wa DDC wenye gharama ya Tshs Milioni 620,000,000.00.

Sheilla, amesema katika Bajeti hiyo idara na vitengo vyote vimezingatiwa lakini kubwa ni pamoja na kuboresha Sekta ya Elimu Sekondari ambapo Manispaa ina shule 50, kati ya hizo 23 ni za Serikali na 27 ni za binafsi huku jumla ya wanafunzi 7,157 walijiunga na shule za Sekondari za Serikali hadi kufikia Januari, 2020 ambapo kati ya hao wavulana 3,484 na wasichana 3,673.
Hata hivyo, amesema kwa mwaka 2019, Manispaa ilipokea Tshs Milioni 571,600,000.00 kutoka Serikali Kuu kupitia Programu ya Lipa kulingana na matokeo (EP4R), ambapo kiasi hicho cha fedha kilitumika kumalizia maboma 34 ya madarasa, ujenzi wa madarasa mapya 7 na matundu 8 ya vyoo.

Pia miongoni mwa sekta zilizoimarishwa ni pamoja na Sekta ya Ardhi, Sekta ya Elimu (msingi na Sekondari), Miundombinu, ujenzi wa maabara za Sayansi, Sekta ya Afya, Sekta ya Mazingira, Utawala bora, Sekta ya Maendeleo ya Ustawi wa Jamii na Vijana, Hali ya Maambukizi ya VVU Katika Manispaa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2019, Mwenendo wa ukusanyaji wa mapato , Sekta ya Ujenzi, Sekta ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika nk.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.