Rai yangu kama mtanzania mpenda maendeleo.
Ndugu zangu napenda kuzungumzia juu ya hali ya uchochezi inayofanywa na baadhi ya makundi na watu wachache wasiokuwa na dhamira njema katika nchi yetu kupitia katika vyombo vya habari kama vile magazeti, mitandao ya kijamii na hata matamko ya hivi karibuni dhidi ya Serikali ya awamu ya tano, napenda kulaani vikali na kwa nguvu taarifa zozote za uchochezi zinazochochea uvunjifu wa amani kitendo kitakachoweza kupalekea kuligawa Taifa letu.
Napenda mtambue tu kwamba kila mmoja wetu ana fursa ya kulitumikia Taifa ili kuchochea kasi ya kuleta maendeleo, hivyo nasikitika sana kuona baadhi ya watu wakitumia muda wao mwingi wa kuchochea uvunjifu wa amani ya nchi badala ya kutumia muda huo kuelimisha jamii.
Viongozi wa dini,asasi za kiraia na kisiasa wana wajibu mkubwa wa kuelimisha jamii juu ya madhara makubwa yanayoweza kutokea ikiwa nchi yetu itaingia kwenye machafuko, kazi kubwa ya Viongozi wa dini ni kuwalea waumini kiroho na kimwili, yapo mambo mengi zaidi yanayoweza kufanywa na wananchi yakaleta manufaa kwa taifa. mfano kufanya kazi kwa juhudi ama katika kilimo ni jambo la busara sana kuliko kuchochea kuleta vurugu zinaweza kupeleka amani ya nchi kupotea.
Endapo amani itapotea hata hao waumini katika dini zao hawatapatikana na wanachama katika vyama vyao hawataonekana , hapatakuwa na utulivu wowote wa kuwahudumia kiroho, kimwili na kisiasa.
Ningependa kujua wapi tulipotoka, tuliko na tunakoelekea kama taifa huru kwani taarifa za upotoshaji wakati fulani zina madhara makubwa kwenye jamii hasa zikiachwa bila kukanushwa na kulaaniwa.
Ndugu zangu, mnafahamu kuwa Historia ya Tanzania imekuwa na awamu nne za utawala na hii ni awamu ya tano , kwa mtazamao wangu na watanzania wengine wenye maono mapana tuna amini kuwa tokea Rais Dkt. John Magufuli aingie madarakani ameweza kufanya mambo makubwa sana, tena kwa muda mfupi hivyo watanzania wenzangu kwa ujumla tunapaswa kumuunga mkono.
Napenda mtambue kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais wetu wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ndani ya muda mfupi imeweza kufufua Shirika la ndege, imerejesha nidhamu ya watendaji Serikalini, imeweza kudhibiti mianya ya rushwa na ufisadi, inatoa elimu bure bila malipo , imeanzisha miradi mikubwa ya ujenzi wa vyanzo vipya vya umeme kama vile Stiglers Gorge utakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 2000 za umeme, mradi wa Standard Gauge yaani Reli ya kisasa ya umeme, Serikali imeweza kuwaondoa watumishi hewa na wenye vyeti feki ili kuboresha utendaji Serikalini, Serikali inafufua Viwanda na kujenga Viwanda vipya kwa mfano kiwanda cha zana za kilimo Kilimanjaro yaani Kilimanjaro Tools, General Tires Jijini Arusha Shirika la usagishaji la taifa yaani NMC, Tanganyika Packesr, kutoa asilimia 10% ya mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kwa kila Halmashauri za Wilaya nchini.
Machinjio ya Kimatafa yanajengwa kwenye ranchi za taifa na ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha Sukari unaendelea Mkoani Morogoro kupitia ubia wa NSSF na PPF na katika miradi hii yote Serikali kwa kiasi kikubwa inatumia fedha za ndani.
Ndugu zangu, Mhe. Rais wetu ameweza kupigana vita kali ya kuhifadhi madini yetu kwenye makinikia na Bunge limeweza kufanya kazi kubwa ya kutunga sheria mpya ya madini na kujenga ukuta mkubwa Mirerani ili kulinda mali zetu, sanjari na hilo Serikali imeanzisha vita kubwa ya madawa ya kulevya na kufungua Mahakama ya mafisadi.
Ndugu zangu, kubwa zaidi Rais Magufuli ameonesha uzalendo uliotukuka kwa kuanzisha vita vya kiuchumi vinavyolenga kulinda maslahi za taifa kama vile madini na hili ndilo limemfanya aweze kuchukiwa na mabepari na mabedui, Rais ameweza kupigana vita kali ya kuhifadhi madini yetu kwenye makinikia na Bunge limeweza kutunga sheria mpya ya madini.
Ndugu zangu, Vyombo vya habari katika dunia ya leo vinachukuliwa kama muhimili wa nne wa dola, hivyo kupitia kalamu za waandishi wa habari tuashirikiane pamoja kuwaelimisha watanzania kuhusu masula haya ili tuweze kulinusuru taifa letu kutoka kwenye mikono ya mabepari hawa na mawakala wao wanaotaka kuliingiza taifa kwenye machafuko. Kwangu na watanzania hatuhitaji hali hiyo itokee kwani imetosha kwa kuwaona wenzetu wanavyoteseka mfano Libya, Iraq, Nigeria na sehemu nyingine kama hizo.
Ndugu zangu, nichukue nafasi hii kuwataka watanzania waelewe kuwa upendo, umoja na mshikamano wetu ndio silaha muhimu ambazo zimekuwa zikitupatia ushindi katika historia ya taifa letu hasa tunapokuwa katikati ya majaribu makubwa , hivi ndivyo vilitupa ushindi wakati wa kupigania uhuru wetu, hivi ndivyo vilitupa ushindi wakati wa vita vya Kagera vya mwaka 1978, hivi ndivyo vilitupatia ushindi tulipoamua kusaidia mataifa ya Afrika kupigania uhuru wao na hivi ndivyo vilitupatia ushindi wakati huu ambapo mabeberu yameamua kutuhujumu waziwazi kwa kuwa tumekataa nchi yetu kugeuzwa shamba la bibi.
Niwaombe Watanzania wenzangu, kamwe tusikubali kuyumbishwa na MAWAKALA wa mabeberu ambao wanatumia saa 24 kutoa taarifa za kutupaka matope ili kuharibu taswira njema ya taifa letu. lazima mjue kwamba Mabeberu wanataka kuvuruga amani ya nchi yetu kirahisi ili yatufike kama yaliyotokea nchini Tunisia mwaka 2011 yatokee kwetu. Wakati haya yakitokea katikati ya ukosefu wa amani ni vita waweza ili waweze kutuibia , kutunyonya na kutukalia kimabavu, kwa jambo hili hatuwezi kukubaliana nalo kamwe.
Mwisho, nipende kuwashukuru sana Waasisi wa taifa letu ambao waliteseka kuhakikisha tunakuwa taifa huru . Ili kuwaenzi wazee hao waliotangulia mbele ya haki kila mtanzania kwa sauti kubwa aseme, mimi ni mzalendo, sitaandamana na yeyote atakayejaribu kuandamana awajibishwe kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Kama ilivyo wapo watu wanaosema wapo tayari kufa kwa kuandamana, hivyo watanzania wazalendo tuhakikishe tunapaza sauti zetu na kupambana na watu hawa wanaotaka kuchafua amani ya nchi yetu na tuwe tayari kwa ajili ya kumuunga mkono Rais wetu Dkt. Joihn Pombe Magufuli kwa maendeleo ya nchi yetu.
"Haiwezekani mpo kwenye boti moja katika bahari akatokea mwenzenu ana kiu cha maji , akaona ni vyema atoboe boti ili apate maji , Ikiwa waliopo kwenye boti watamwachia atoboe boti ni dhahiri maji yataingia kwenye boti na litazama na wote watakufa"" Hivyo hatupo tayari kuona jambo hilo linatokea nchini kwetu kwa watu wachache kwa maslahi yao kutaka kuchafua amani ya nchi yetu.
Kwa pamoja kwa wale watanzania wenye mapenzi mema na nchi yao tutoe ahadi ya utii na unyenyekevu kwa Amir Jeshi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli katika kulinda na kudumisha amani na rasilimali za Taifa letu.
“Kwa nchi yoyote duniani, umoja na amani ni nguvu kubwa. Kwa nchi changa na maskini kama yetu, umoja na amani ni amana na tunu kubwa isiyo na bei. Tukiulizwa na wenye kiburi na fidhuli ya wingi wa mali: mna nini nyinyi Watanzania? Tunaweza kujibu, si kwa fidhuli, lakini kwa fahari kabisa: tuna amani na umoja vitu ambavyo havinunuliki kwa kiasi chochote cha pesa.”Nukuu ya Mwalimu Nyerere kulinda umoja na amani
Imeandikwa na Yusuph Mwamba Mchambuzi wa masuala ya Siasa.
Post a Comment