MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO ATAKA MWALIMU NYERERE AENZIWE KWA VITENDO
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba. |
VIONGOZI wa vyama vya Siasa wametakiwa kuiga kwa vitendo uzalendo na moyo wa kujitoa aliokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake ili kuliwezesha Taifa kupiga hatua kimaendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, wakati akiendelea kuweka msisitizo wa nidhamu kazini .
Ameeleza kuwa maisha aliyoishi Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa na viongozi na watanzania wote hasa pale alipojitofautisha na viongozi wengi wa Bara la Afrika alipoepuka tamaa ya madaraka na mali kwa manufaa ya taifa.
“Serikali yetu ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Dkt John Magufuli imekuwa katika mstari wa mbele kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo , hata mimi napenda kusisitiza uwajibika,uzalendo,uandilifu na nidhamu katika kulitumikia taifa la Tanzania kama mnakumbuka mwalimu alikuwa anapenda kutumia neno (it can be done play your part) kila mtu atimizi majukumu yake” Amesema Sheilla.
Amesema kuwa kumbukumbu za Baba wa Taifa zilizohifadhiwa vizuri katika makumbusho hiyo zina mambo mengi ya kujifunza ambayo wanasiasa wanatakiwa kuyafanya kwa vitendo hasa uzalendo kwa nchi, uvumilivu, upendo na moyo wa kujitoa kwa dhati kuwatumikia wananchi.
“Kupitia kumbukumbu hizi sisi watumishi tumejifunza ukomavu wa demokrasia aliokuwa nao Mwalimu Nyerere akiwa ndani na nje ya Bara la Afrika, wengi wanadhani Demokrasia ni wakati wa uchaguzi tu, kumbe demokrasia ni pamoja na kuheshimu watu wengine,sote ni mashahidi kupitia kumbukumbu zake tumeona mahali alipokuwa anaishi mwalimu kabla hajajengewa nyumba na Jeshi kama Rais mstaafu wengi walitegemea asingeishi katika eneo lile, kumbukumbu hii nzuri aliyoiacha inatufundisha watanzania kuwa mwalimu aliitanguliza Tanzania mbele kuliko maslahi yake binafsi” Amesisitizia Sheilla.
Sheilla, amebainisha kuwa serikali itaendelea kumuemzi Baba wa Taifa kwa yale aliyoyafanya na kuyasimamia kwa manufaa ya taifa huku akitoa wito kwa viongozi wa vyama vya Siasa wawe na kiasi na waridhike na vile walivyonavyo.
Amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kumuenzi vyema Mwalimu Nyerere katika kuimarisha misingi mizuri ya kazi ikiwamo uaminifu, uadilifu na kupinga vitendo vyote vya rushwa pamoja na kuibua miradi mikubwa itakayoiletea Tanzania maendeleo makubwa kuelekea uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda.
Aidha, amemalizia kwa kuwataka watendaji wote wa serikali ya Halmashuri ya Manispaa ya Morogoro, kufanya kazi kwa uaminifu,uadilifu,kuwajibika kwenye majukumu yao na kujituma na kamwe hata kuwa tayari kuwavumilia watendaji ambao ni wazembe kazini.
Post a Comment