Changamoto Dampo Manispaa ya Morogoro yapatiwa ufumbuzi.
Burudozer (mtambo), kilichokodiwa na Manispaa ya Morogoro kikiwa kazini Dampo kwa ajili ya kuweka njia za kupitia magari ya taka . |
Njia mbadala za kuingilia magari ya taka baada ya kusawazisha vifusi vya taka vilivyojazana katika dampo hilo. |
Afisa afya na msimamizi wa dampo, Msisa Ziota, akionesha mtambo wa Manispaa ambao upo katika matengenezo. |
Dampo likionekana kuwa safi baada ya mtambo wa kijiko kusawazisha takataka na kuzisambaza katika Dampo hilo ili kuweka njia za magari kuingia ndani. |
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya
Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kero ya Dampo kwa sasa inakwenda kumalizika
kufuatia kuweka kijiko kitakacho safisha njia na kuingiza takataka zote ndani
ya Dampo hilo.
Akizungumza kuhusu kero hiyo, amesema kwa sasa
kazi imeshaanza ya kuweka njia mbadala ambazo zitarahisisha magari ya taka
kuingia katika dampo na kumwaga uchafu jambo ambalo awali lilikuwa changamoto
kutokana na taka kutupwa nje ya dampo na kupelekea kero za kimazingira kwa
wananchi.
"Ili kuondoa kero kwa wananchi ya harufu ya
dampo na inzi wengi tumechukua uamuzi wa kukodisha kijiko kwa muda ili kuweka mazingira mazuri
ya kuhakikisha takataka zote zinaingia ndani ya dampo, vifaa vyetu bado
vinachangamoto lakini navyo tunavishughulikia vipo katika matengenezo, niwahakikishie
Wananchi wa Manispaa ya Morogoro hakutazagaa takataka tena katika mitaa yetu na
katika makazi ya wananchi , kwani magari yapo na dampo letu linaingilika kwa
urahisi tofauti na awali " Amesema Sheilla.
Amesema
kuwa, dampo hilo limekuwa likilalamikiwa nakusababisha uchafu kuingia
mpaka barabarani na kusogea karibia na maeneo ya kazi za watu huku harufu mbaya
ikiendelea kuwa kero kwa watu kila siku.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Manispaa ya
Morogoro, Samweli Subi, amesema kuwa
suala la uchafu katika Manispaa lipo ila
jitihada
zinafanyika ili kupambana na suala la uchafu ambapo amewataka wale wanaohusika
na ukusanyaji wa taka majumbani na mitaani wazidishe kasi kwani kwa sasa dampo
hilo linapitika kirahisi tofauti na mwanzo.
Pia, amewataka wananchi kuhakikisha wanaweka
mazingira safi na salama kwani Manispaa imejitahidi kununua mapipa ya
kuhifadhia taka na kuyasambaza maeneo tofauti tofauti wakiwa na lengo la kuweka manispaa safi kwa ajili ya afya za
wananchi wake.
Naye ,
Afisa afya na msimamizi wa dampo, Msisa Ziota, amemshukuru Mkurugenzi wa
Manispaa kwa jitihada za kupata Kijiko mbadala cha kuchonga njia mbadala za
kupitishia magari ya taka.
Amesema Kijiko hicho kipo kazini na tayari
wameshaanza kuweka njia nzuri na magari ya taka yanaweza kuingia na kutupa taka
katika dampo hilo kwa urahisi tofauti na awali
"Hatua nzuri sana, mwanzo hali ilikuwa mbaya
takataka zote zilikuwa zinabakia nje nyingine zinaleta harufu katika makazi ya
watu nzi wanazaliana wengi hususani katika kipindi cha mvua harufu inakuwa kali
baada ya taka kuoza lakini kwa sasa magari yanapita kilichobakia ni kuweza
kupata Wheel Loader ili kuchota taka zilizo pembeni mwa barabara na kuziingiza
ndani baada ya hatua za awali ya kuzisogeza pembeni kuweka njia ya magari
kupita"Amesema Ziota.
Post a Comment