RC Sanare aridhishwa na mwitikio wa Wananchi uandikishwaji Daftari la kudumu la Wapiga Kura.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, amefurahishwa na idadi ya watu wanaoendelea kujitokeza kujiandikisha katika vituo mbalimbali vya Uandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga katika Jimbo la Morogoro Mjini lilopo Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro.
RC Sanare ametumia fursa hiyo kuwasisitiza vijana na wale wanaorekebisha taarifa zao kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kama hajajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ama hana kadi ya mpiga kura.
Hata hivyo, RC Sanare, amewahimiza vijana waliotimiza miaka 18 na wale ambao mwaka huu mwezi Oktoba wanatarajia kufikisha umri huo wa miaka 18 wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili kutimiza haki yao ya kuwachagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Nitoe rai kwa vijana wote wa Kitanzania waliotimiza umri wa miaka 18 au wale ambao watatimiza umri huo ifikapo Oktoba, 2020 wajitokeze kwa wingi na kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hawa ndio walengwa wakuu kwa sababu wanaingia kwa mara ya kwanza katika uchaguzi,ikumbukwe kwamba, bila kujiandikisha hawataweza kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka, hivyo kujiandikisha kwao kutawahakikishia ushiriki wao katika uchaguzi wa viongozi "Amesema RC Sanare.
Amesema watakaohusika awamu hii ni wapiga kura waliotimiza miaka 18 hivi karibuni, wale watakaotimiza miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, waliohama kata au jimbo na kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi.
Wengine ni waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa sambamba na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki.
Zoezi hilo la Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura, linafanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo llitafanyika nchi nzima na linatarajiwa kukamilika Machi, 2020.
Amesema ana imani kuwa wananchi wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama inavyoendelea kutolewa, basi watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba ya kujiandikisha katika daftari hilo na hatimaye kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Amewataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ambayo itawapa fursa ya kuwachagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika ockoba mwaka huu.
Sheila Lukuba ni mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro sio afisa mwandikishaji
ReplyDelete