Header Ads

Rais wa Zanzibar Dkt Shein aelezea adhma ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri juu ya kuendelea kuiunga mkono nchi yake katika kuimarisha Sekta ya Kilimo




RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  ameipongeza azma ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini.

Hayo aliyasema leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Masuala ya Ardhi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Dk. Ezzaldin Abusteit ambapo katika mazungumzo hayo Waziri huyo pia, aliahidi kushirikiana na Zanzibar katika kuliimarisha na kuliendeleza shamba la pamoja na Kilimo la JKU- Bambi, liliopo Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa Misri imekuwa  mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo kilimo ambayo ni sekta muhimu katika maisha ya Wazanzibari.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa azma ya Serikali ya Misri ya kuendeleza mashirikiano katika uendelezaji wa mradi wa Shamba la pamoja la JKU-Bambi ambalo ni ushirikiano kati ya nchi hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeweza kuleta tija na maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo.

Alieleza kuwa miongoni mwa mafanikio yaliopatikana ni pamoja na kuwepo kwa wataalamu na utaalamu unaotokana na msaada wa Misri ambapo juhudi hizo zimeweza kusaidia kwa kiasikikubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini hasa katika mradi huo.

Hivyo, katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza ushirikiano huo sambamba na kuzidisha mikakati kwa kuendeleza tafiti za pamoja katika sekta hiyo kwa lengo la kuzidisha uzalishaji, mbegu, aina za udongo na tafiti nyenginezo kwenye vianzio vya kilimo.

Aidha, Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa katika kuliendeleza na kuliimarisha Shamba hilo sambamba na Serikali ilivyojipanga katika masuala ya utafiti wa kilimo ikiwa ni pamoja na kuipa kipaumbele taasisi ya utafiti pamoja na Chuo cha Kilimo kiliopo Kizimbani.

Alieleza kuwa kwa upande wa chuo hicho cha Kilimo, tayari kimeshaungwanishwa na Chuo Kikuu cha Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa lengo la kupata mafanikio zaidi katika utoaji wa taaluma ndani ya sekta ya kilimo.


Rais Dk. Shein alisema kuwa tayari mwanzo mzuri umeanza kuonekana katika  mashirikiano ya uendelezaji wa sekta hiyo ya kilimo kati ya Misri na Zanzibar na kusisitiza haja ya kuuendeleza ushirikiano huo ili uzidi kuleta mafanikio kwa pande zote mbili.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.