Header Ads

Rais wa Zanzibar aahidi kuimarisha huduma za Maendeleo kisiwa cha Uzi

















RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa si muda mrefu kisiwa cha Uzi kitafumbuka kwani Serikali anayoiongoza itahakikisha inaimarisha huduma za maendeleo ikiwemo kujenga barabara na daraja kutoka Unguja Ukuu Kaepwani hadi Uzi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ziara yake ya Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja wakati alipotembelea kisiwa cha Uzi na kuweka jiwe la Msingi katika Skuli ya Maandalizi na Msingi ya Ng’ambwa na baadae kuwahutubia wananchi wa Uzi.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mipango kabambe ya kuhakikisha wananchi wa Kisiwa cha Uzi wanapata huduma zote muhimu kwa uhakika ikiwemo usafiri wa barabara, Skuli ya Sekondari pamoja na kuimarisha huduma za masi safi na salama.

Alieleza kuwa barabara ya Kutoka Unguja Ukuu Kaepwani hadi Uzi kwa kujengwa daraja linalokadiriwa kuwa na urefu wa mita 400 inawezekana kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshatekeleza miradi mikubwa kuliko huo.

Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wa kisiwa hicho kufanya subira kwani Serikali itajenga daraja hilo kuelekea usawa wa bahari hatua ambayo itawaondoshea wananchi wa kisiwa hicho usumbufu wa usafiri wa barabara.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar inampango wa kukopa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya ya Afria AfDB kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika kisiwa hicho cha Uzi ambao utaondoa kabisa uhaba wa huduma hiyo.

Akieleza kuhusu azma ya Serikali kuimarisha sekta ya elimu katika kisiwa hicho cha Uzi, Rais Dk. Shein ameeleza kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inajenga Skuli ya Sekondari ya Uzi Ng’ambwa pamoja na kupeleka samani.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.