Rais wa Zanzibar awapongeza UWT kufanya Kongamano la utekelezaji wa Ilani ya CCM kipindi cha miaka 3
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza azma ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kufanya Kongamano la Kitaifa la kupongeza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)kwa kipindi cha miaka 3 ya uongozi wake.
Hayo aliyasema leo wakati alipokutana na uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wakiwemo Wajumbe wa Kamati Tekelezaji ya Umoja huo Ikulu mjini Zanzibar ambapo Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kupongeza rai na azma hiyo ya Umoja huo wa (UWT).
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar alieleza kuwa Kongamano hilo litatoa mwanga katika kutambua juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea kutekeleza majukumu yake ambayo ni pamoja na kuimarisha miradi ya maendeleo Unguja na Pemba, mjini na Vijijini kwa manufaa ya wananchi wote ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani hiyo ya CCM.
Hivyo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza Umoja huo kwa kufikiria kufanya jambo hilo muhimu ambalo litatoa taswira nzuri kwa jamii ambayo inatambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali yao katika kuwaletea maendeleo endelevu.
Aidha, Rais Dk. Shein alipongeza kwa maandalizi ya Kongamano hilo ambalo litaanzia Kisiwani Pemba na baadae kufanyika Unguja huku akisisitiza haja ya kuendelea kuungwa mkono Jumuiya hiyo ili izidi kuimarika na kuleta mafanikio kwa Taifa.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendelezwa kwa umoja na mshikamano ndani ya Jumuiya hiyo ambayo imeweza kupata mafanikio makubwa na kuimarika zaidi tokea kuanzishwa kwake.
Post a Comment