Header Ads

WATENDAJI WA MITAA MANISPAA YA MOROGORO WAMETAKIWA KUZINGATIA LISHE BORA KWA WANANCHI.


MAAFISA  Watendaji wa Mitaa Manispaa ya Morogoro ,  wametakiwa kuzingatia mkakati wa Serikali juu ya masuala ya Lishe bora ya wananchi katika maeneo yao, kupitia mkataba wa Lishe uliosainiwa na Watendaji wa Kata , lengo likiwa kuondoa hali ya udumavu katika jamii na kuwa na jamii yenye afya bora.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Afisa Utumishi Manispaa ya Morogoro, Shabani Duru, wakati akifungua kikao kazi cha mkatati wa hali ya lishe, Mkataba wa lishe pamoja na maandalizi ya Siku ya Lishe Duniani.

Kikao hicho chenye  lengo la kufanya tathmini ya hali ya lishe , kimefanyika  kwenye ukumbi wa mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa Machi 25/2024.

Duru , amewaagiza watendaji hao, kuwa na mkakati shirikishi, utakaowashirikisha wananchi, Wahudumu wa Afya, wahudumu wa Afya ngazi ya jamii pamoja na wadau wa maendeleo, kutoa elimu ya Lishe kwa jamii, ili kuhakikisha wananchi wote wanapata ufahamu juu ya lishe bora, hususani kwa wajawazito na watoto.

“Ninawagiza watendaji wote, Lishe iwe agenda ya kudumu katika vikao vyenu vyote  kwenye maeneo yenu, hakikisheni hata haya mafunzo mnayopewa na mikakati yenu muende mkawashirikishe  waheshimiwa Madiwani, lengo likiwa kuondoa udumavu wa mwili na akili kwa wananchi wote maeneo yotu, kupitia tathmini ya miaka iliyopita tangu tusaini mkataba wa lishe Manispaa tumefanya vizuri niombe tuanze tulipo ishia twendeni tukafanye  vizuri zaidi ” Amesema Duru.

Aidha, Duru,  amewasisitiza Watendaji hao, kuhakikisha kina mama Wajawazito katika maeneo yao wanapata Lishe bora katika siku 1000 za ujauzito, lishe ambayo tafiti zinaonesha ndio inawezesha mtoto aliye tumboni kujenga afya bora ya ubongo na mwili, afya ambayo ndio inategemewa na jamii na Taifa hapo baadaye na kuwasisitiza kutumia vyakula kutoka makundi matano ya vyakula, vyakua ambavyo vinapatikana katika maeneo yote ya Manispaa ya Morogoro.

Naye Mkuu wa Kitengo cha huduma za Lishe  Manispaa ya Morogoro, Ester Kawishe, amewataka Maafisa watendaji hao, kuhakikisha wajawazito wote katika maeneo yao wanahudhuria kliniki pindi wanapopata ujauzito, wazazi wote wenye watoto wa umri chini ya miaka mitano kuwapeleka watoto hao kliniki, pamoja na kupiga vita tabia ya kina mama wajawazito kujifungulia nyumbani sambamba na kuweka sheria ndogo za kuwashughulikia wale watakaokiuka.

“Ninawasisitiza Maafisa Watendaji wote wa kata na vijiji kufanya kazi kwa kushirikiana kama timu, ili kuhakikisha wananchi wenu wanakula vyakula kwa kuzingatia makundi yatakayowapa lishe bora, wananchi wakiwa na afya bora nguvu kazi itaongezeka na wananchi wakiwa na nguvu, wataleta maendeleo katika maeneo yetu”Amesema Kawishe

Watendaji waliohudhuria kikao kazi hicho, wamekiri kupata uelewa mkubwa juu ya masuala ya Lishe, na kuahidi kwenda kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na serikali  na wataongeza kasi ya kuhakikisha wajawazito wanahudhuria kiliniki na wenza wao, pamoja na kuwapatia lishe bora katika siku 1000 za ujauzito, siku ambazo zinaonekana kuwa ni msingi wa afya ya binadamu yoyote.

Awali serikali imeandaa mpango wa Lishe wa miaka mitano 2022 -2027, unaotaka kila mwananchi kuwa kupata lishe bora kwa kula mlo wenye makundi matano ya vyakula kuanzia siku 1000 za mama mjazito, mtoto anapozaliwa mpaka miaka mitano na jamii nzima, mkakati unaoelekeza kuwasainisha mikataba Maafisa Watendaji wa Kata ili kusimamia mkakati huo wa Lishe.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.