Header Ads

ABOOD AGEUKA MBOGO SUALA LA KUSOMA MAPATO NA MATUMIZI KWENYE MITAA

 



MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Dkt. Abdulaziz Abood, amewaomba Watendaji wa Kata na Mitaa Manispaa ya Morogoro kusoma taarifa za Mapato na Matumizi kwa Wananchi ili kuweza kuondoa wasiwasi kwa Wananchi juu ya matumizi ya Pesa zinazotolewa kwa ajili ya Maendeleo.

Hayo ameyazungumza katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Mzinga na Kauzeni Machi 22/2024 sambamba na kutembelea miradi ya maendeleo katika Kata hizo.

Sambamba na hayo, Mhe. Abood,  amewaomba Madiwani kuwa na ushirikiano ili kuleta maendeleo katika Kata zao na wananchi kuona matunda ya viongozi wao .

 “Naomba muwe na mahusiano mazuri mpendane ili muweze kufanya kazi kwa pamoja hata kupelekea maendeleo katika kata zenu maendeleo huja kwa kushirikiana” Amesema Mhe. Abood.

Nao Madiwani wa Kata zote mbili Kauzeni na Mzinga, wamemuhakikishia Mhe. Abood kuwa maagizo yote, ushauri watayafanyia kazi kikamilifu ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Katika hatua nyingine , Mhe. Abood, amewaagiza MORUWASA kutoweka ratiba za mgao wa  maji katika Kata hizo kwani wana mradi mkubwa ambao uliombewa kuondoa changamoto za maji.

" Hili la mgao wa maji sikubaliani nalo, hapa tumeleta mradi mkubwa wa maji ambao tumeona utasaidia changamoto za maji , nashangaa kuona leo kuna mgao , nikuombe Mkurugenzi  wa MORUWASA najua mna utaratibu mzuri wa kufunga mita kwa kila mwananchi, niombe kamilisheni taratibu zenu zote mkiwa tayari sasa  mnaweza kukaa chini na wananchi hawa mkakubaliana njia sahihi ya upatikanaji wa maji lakini kwa sasa mgao acheni" Amesema Mhe. Abood,

Aidha, Mhe. Abood, amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Manispaa ya Morogoro miradi mikubwa ya Kimkakati  kwani amegusa sehemu zote afya, elimu na sasa anaelekeza nguvu katika suala la miundombinu ya barabara.

Mbali na barabara, Mhe. Abood, amewataka wale wote waliohusika na utafunaji wa fedha za kupanua mto Kata ya Mzinga wahakikishe  wanazirudisha kwani hata wavumilia.

Naye Diwani wa Viti Maalum Kata ya Kauzeni, Mhe. Salma Mbando, amesema Kata ya Kauzeni katika kipindi cha Miaka 3 ya Rais Samia , imepokea zaidi ya Milioni 900 jambo ambalo halijawahi kutokea katika vipindi vya nyuma.

" Mhe. Abood, tufikishie salamu kwa Rais wetu, mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani Manispaa yetu tumenufaika sana na fedha zake na miradi ya maendeleo inasonga mbele, na wewe pia umekuwa mfano wa Wabunge katika Manispaa yetu , wapo wametangulia lakini wewe umefunika , fedha zako za mfuko wa Jimbo zimetusaidia sana, Shule yetu ya Msingi Kauzeni ilikuwa na uhaba wa matundu ya Vyoo lakini mpaka muda huu tuna upungufu wa matundu 3 hiyo ni hatua kubwa sana" Amesema Mh. Mbando.

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Mzinga, Mhe. Salum Chunga, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa ujenzi wa Shule ya kisasa ya Sekondari ambapo wanafunzi walikuwa wanasafiri umbali mrefu kwenda shule ya Sekondari Kauzeni lakini kwa sasa wamerahisishiwa huduma hiyo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.