Header Ads

FIFA KWA KUSHIRIKIANA NA TFF YAKABIDHI MIPIRA 240 MANISPAA YA MOROGORO KUTEKELEZA PROGRAMU ZA MICHEZO SHULENI.















SHIRIKISHO la Mpira  wa Miguu Tanzania (TFF)  kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA , limekabidhi mipira 240  kwa shule za msingi 6 Manispaa ya Morogoro  kwa lengo la kutekeleza programu za michezo shuleni.

Makabidhiano ya mipira hiyo yamefanywa Machi 06/2024  na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ,Mhe. Rebecca Nsemwa, akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro mipira hiyo kwa ajili ya kuwagaia waalimu wa michezo wa shule hizo 6 ambazo zimekuwa kipaumbele kwa awamu ya kwanza.

DC Nsemwa,  ameishukuru TFF, ambapo ameagiza kila shule ambayo imepokea mipira kuhakikisha inatumika kwa watu sahihi.

Aidha, DC Nsemwa, amesema wana uhakika  kupitia mipira hiyo, wanakwenda  kuibu vipaji halisi, kwani ukosefu wa mipira ilikuwa changamoto kubwa, hivyo wanaishukuru  TFF na FIFA kwa kutatua changamoto hiyo.

“ Sitegemei kuona au kusikia mipira hii inatumiwa na watu wazima, hii mipira imetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi, darasa la kwanza hadi saba, tunataka kuona Manispaa ya Morogoro  tunatoa akina Samatta wengi,” Amesema DC Nsemwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro , ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema kuwa ya utoaji wa mipira mashuleni  imeanzishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ikiwa ni mbadala wa programu ya grassroot ambapo lengo lake ni kukuza vipaji kwa wanafunzi.

Kihanga,amesema  mipira hiyo imekuja katika wakati mwafaka, kwani FIFA na TFF wamedhamilia kuibua vipaji kuanzia ngazi za chini.

“Ni matumaini ya Rais wetu wa TFF kuwa mipira hii inakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa, tunataka kuona vipaji vinaibuliwa kupitia mipira hii, TFF na FIFA watakuwa wanakuja kufanya ukaguzi kuona kama mipira hii inaleta tija,” Amesema Mhe. Kihanga.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Andreas Whero , amemshukuru Rais wa TFF Wallace Karia kwa kuchagua MManispaa ya Morogoro  kuwa miongoni mwa Manispaa ambazo zimechaguliwa  kupata mipira .

Whero, amesema kuwa kwa kushirikiana na Menejimenti ya Manispaa na waalimu wa michezo mashuleni ,amesema  atahakikisha kuwa mipira hiyo inaleta tija na shule ambazo zimepatiwa mipira hiyo zinakwenda kuibua  vipaji  kupitia vifaa hivyo.

Naye ,Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Johnerick Fredirick Alfred... amesema kuwa  jumla ya shule 6 Manispaa ya Morogoro zimepatiwa  mipira hiyo, ambapo kila shule imepata  mipira 40  ambapo wanafunzi wataitumia wakati wa michezo.

Shule zilizopatiwa mipira ni Shule ya Msingi Mwere , Mindu, Maghorofani , Kingolwira, Bungo na Mafiga.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.