Header Ads

MZERU AWATAKA WANAWAKE KUMUUNGA MKONO RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Norah Mzeru, amewataka wanawake katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuwa mstari wa mbele kumuunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kazi kubwa anayoifanya kuleta maendeleo kwenye jamii na kuboresha upatikanaji wa huduma.

Kauli hiyo ameitoa Machi 10/2024 katika hafla ya pamoja ya wanawake iliyoandaliwa na Kituo cha habari cha Planet FM chini ya Mkurugenzi wa Vipindi , Bi. Warda Makogwa kwenye Ukumbi wa Mount Uruguru Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na wanawake waliojitokeza katika hafla hiyo, Mhe. Mzeru, amesema  kuwa  Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amekuwa akianzisha harakati nyingi zenye lengo la  kumkomboa mwanamke kiuchumi.

" Rais wetu anapambana kuhakikisha wanawake wananyanyuka kiuchumi  lakini hata hizi program ambazo nchi yetu imekuwa ikizifanya juu ya wanawake ni program zenye tija ukiziangatia  Tanzania ipo katika jitihada za kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi" Amesema Mhe. Mzeru.

Mhe. Mzeru, amesema  Tanzania ni mojawapo ya Mataifa yanayotekeleza malengo ya Jukwaa la Kimataifa ya Kukuza usawa wa Kijinsia ambapo katika hilo  Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara wa utekelezaji wa Jukwaa hili hususan kuhusu Haki na Usawa wa Kiuchumi.

Aidha, amewataka wanawake kuendelea  kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya  kazi kwa bidi na kuwa na  biashara zenye tija na zenye ushindani kimasoko.

" Nimevutiwa na kauli mbiu ya mwaka huu 2024 “ WEKEZA KWA WANAWAKE KUHARAKISHA MAENDELEO YA TAIFA NA USTAWI WA JAMII” niwaombe wanawake wenzangu  wale ambao ni wajasiriamali basi tuhakikishe tunapowekeza basi bidhaa zetu ziendanane na ubora wa uwekezaji ili kuleta ushindani wa masoko hapo tutakuwa tunafanya uharakishaji wa kuuza bidhaa na tutaleta maendeleo chanya kwa Taif ana Ustawi wa Jamii" Ameongeza Mhe. Mzeru.

Mbali na yote aliyozungumza, amesema  kuna wimbi la unyanyasaji wa kijinsia na ubakwaji kwa Watoto, huku akisisitiza hayo mambo siyo ya kuyafumbia macho na kuwataka wazazi/ walezi  kuwa karibu na watoto wao mara kwa mara na sio kuwaachia  waalimu kwani wazazi ni sehemu ya msaada ya kumlinda mtoto ili atimize malengo yake.

Mwisho, amewashukuru  sana Planet FM kituo bora kabisa cha habari nchini kwa kuandaa tukio hilo la kuwakutanisha wanawake shupavu , huku akiiomba Planet FM waanze  kuwafikiria  wajasiriamali wa chini angalau kuwapatia  vipindi mara moja bure hata cha dakika 5 ili wajitangaze na baadae waje kuona Fahari ya kuwa na meneja mwanamke wa kituo cha Habari. 

Naye Mkurugenzi wa vipindi Planet FM , Bi. Warda Makongwa, amempongeza Mhe. Mzeru kwa kufika katika sherehe yao huku akimuomba kuangalia namna ya kuwainua wajasariamali wa chini ili wanyanyuke kiuchumi.

Makongwa, amesema wameandaa hafla hiyo kwa wanawake wasioendeshwa na mfumo dume ili wazidi kupeana fursa mbalimbali kwa ustawi wa Jamii na kuharakisha maendeleo ya Taifa kama kauli mbiu ya siku ya wanawake inavyosema.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.