Header Ads

MACHELA AGA RASMI MANISPAA YA MOROGORO , AMSHUKURU RAIS SAMIA SULUHU KUMUAMINI KATIKA UONGOZI WA SERIKALI YAKE


ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kumwamini na kumpa uongozi wa kiutendaji katika Manispaa ya Morogoro na kwa sasa anakabidhi kijiti kwa Mkurugenzi mpya.

Hayo amesema katika tukio la makabidhiano ya Ofisi ya Ofisi na Mkurugenzi Mpya wa Manispaa ya Morogoro, Ndg. Emmanuel Mkongoyaliyofanyika Ofisi ya Mkurugenzi Machi 26/2024.

Hata hivyo , Machela, ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro pamoja na kuwashukuru  watumishi wa Halmashauri hiyo kwa ushirikiano katika kazi kuanzia alipoteuliwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na sasa anakabidhi kijiti kwa Uongozi mpya.

“Leo tarehe 26/03/2024 , nafarijika sana kukabidhi Ofisi hii nikiwa nafuraha tele kwani katika utendaji wangu wa kazi, watumishi wenzangu walikuwa wananipa ushirikiano wa kutosha , Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi ngazi ya Wilaya na Ofisi ya Mbunge wetu wa Jimbo la Morogoro Mjini , tulianza safari salama kwa kufanikisha miradi mingi ya maendeleo na viporo vya muda mrefu ambavyo nilivikuta vimesimama , tumefanya vizuri sana katika Sekta ya elimu na afya, niombe watumishi mnaobakia hapa , mmepata kiongozi mpya muendelee na ushirikiano wenu kama mlivyokuwa mkinipatia mimi ili mtimize ndoto yenu ya kuwa Jiji" Amesema Machela.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amemshukuru aliyekuwa , aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,  Ally Machela, kwa kufanya makubwa sana katika Manispaa ya Morogoro, hivyo kuwaomba watumishi waliopo kumuunga mkono Mkurugenzi mpya kwa kuwa na  mbinu mpya ya kuhakikisha kazi na majukumu ya Halmashauri  yanaenda kwa pamoja na kwa mafanikio makubwa.

“Mkitoka hapa mkaongeze jitihada za kufanya kazi, ili tusivuke na miradi hiyo kwa mwaka wa fedha mpya 2023/2024, tufanye kazi kama timu, niombe Mkurugenzi mpya kauli yetu kwa sasa ni Jiji tarajiwa tunaomba kwa maarifa yako utuvushe twende huku tunapo pataka , pia hakikisha kwa kushirikiana na timu yako ya CMT kipaumbele chenu ni kukusanya mapato ili ndoto ya Jiji itimie na tuweze kutoa huduma bora kwa wananchi wetu" Amesema Mhe. Kihanga.

Kwa upande wa Mkurugenzi mpya, Ndg. Emmanuel Mkongo, ameomba ushirikiano kwa watendaji wote  hasa katika utatuzi wa changamoto ili Manispaa ya Morogoro iweze kusogea mbele zaidi na kutimiza adhima ya kuwa Jiji.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.