KIHANGA AGAWA MIPIRA 27 KWA VILABU VYA SOKO WILAYA YA MOROGORO
MWENYEKITI wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amegawa jumla ya mipira 27 kwa Vilabu 27 Wilaya ya Morogoro .
Tukio hilo la kugawa mipira limefanyika Machi 30/2024 mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Viongozi wa Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Morogoro kwenye Ukumbi wa DDC Mbaraka Mwishehe Manispaa ya Morogoro ambapo Ndg. Selestin Mbilinyi ameibuka mshindi na kuwa mwenyekiti mpya wa Wilaya.
Kihanga, ameagiza Vilabu vyote ambavyo vimepatiwa mipira hiyo vihakikishe kuwa mipira ambayo wamepokea inatumika kwa watu sahihi.
“ Sitegemei kuona au kusikia mipira hii inatumiwa na watu wazima, hii mipira ni kwa ajili ya watoto chini ya miaka 20 , tunataka kuona vipaji vya uhakika , turejeshe morogoro ya enzi , asilimia kubwa ya wachezaji wetu Simba na Yanga wengi ni zao la Morogoro hivyo tuendelee kuzalisha vipaji vingi zaidi michezo ni ajira " Amesema Kihanga.
Aidha, Kihanga, amesema katika Uongozi wake kwa awamu hii ya sasa amekuja kivingine kwani dhamira yake ni kutaka kuibua vipaji kuanzia ngazi za chini.
“Ni matumaini yangu hii mipira ambayo nimewapatia Vilabu vyetu vya Wilaya inakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa, tunataka kuona vipaji vinaibuliwa kupitia mipira hii, mimi na timu yangu tutashuka huko chini kufanya ukaguzi kuona kama mipira hii inaleta tija, lakini walengwa haswa ni wale wenye umri wa chini ya miaka 20 ” Ameongeza Kihanga.
Kihanga, amesema hakuishia tu kwenye Vilabu kwani mipira hiyo pia ameigawa Shuleni ikiwa na lengo la kukuza vipaji kwa wanafunzi.
Post a Comment