Header Ads

DIWANI NDWATA KUKARABATI BARABARA YA KIHONDA SEKONDARI KWENDA MTAA WA MSAMVU



DIWANI  wa Kata ya Kihonda Maghorofani Manispaa ya Morogoro , Mhe. Eng. Hamisi Ndwata  ameungana na wananchi wa Kata ya Kihonda Maghorofani hususani Mtaa wa Msamvu  katika kukarabati miundombinu ya barabara inayotokea Kihonda Sekondari kwenda Mtaa wa Msamvu ili iweze kupitika vizuri na kuchochea maendeleo ya jamii.

Akizungumza  na baadhi ya wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo la umwagaji wa vifusi vya kokoto, Eng. Ndwata, amesema, barabara hiyo imekuwa barabara korofi  ambayo licha ya jitihada walizofanya awali bado inaonekana kuwa kizungumkuti.

Eng. Ndwata, amesema watumiaji wa barabara hiyo wamekuwa wakipata shida sana hivyo kama kiongozi ameona achukue hatua ya kukarabati barabara hiyo.

“Hii ni miongoni mwa barabara zenye shida sana, awamu hii ya kwanza tumeona tuweke vifusi vya mawe kwanza kisha baada ya mvua kukata tutaanza rasmi sasa kusambaza pamoja na kuchimba mitaro ya barabara, wenzetu wa TARURA wapo hapa na wametuhakikishia kuwa baada ya mvua watatupatia mchango wa mafuta na sisi jukumu letu ni kutafuta Lori ambalo litakuwa na kazi ya kusambaza vifusi, hizi ni fedha zangu mwenyewe kama Diwani na ninafanya hivi kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi wangu hususani wanaopita na vyombo vya moto " Amesema Eng. Ndwata.

Naye Meneja wa TARURA Manispaa ya Morogoro, Eng. Mohamed Muanda, amempongeza Eng. Ndwata kwa kuwapambania wananchi wake husuani katika huduma muhimu sana ya miundombinu ya barabara .

" Mh. Diwani alituomba tufike hapa  na tumeona tatizo la barabara lilivyo , sisi kama TARURA tunacho muahidi kwetu mara baada ya mvua kukata tutamsaidia mafuta na wataalamu wetu wa barabara watakuwepo hapa kuhakikisha barabara hii inatengamaa na inakuwa imara ili ipitike vizuri " Amesema Eng. Muanda.

Nao wananchi waliofika katika umwagaji wa vifusi ya barabara hiyo, wamempongeza Mhe. Diwani kwa jitihada zake za kuhakikisha miundombinu ya barabara katika Kata yake inakuwa bora huku wakiwahimiza  wananchi wote kushirikiana na Diwani kuweza kufanya ukarabati wa barabara zenye changamoto zilizopo katika Kata ya Kihonda Maghorofani.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.