MBILINYI MWENYEKITI MPYA CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU WILAYA YA MOROGORO
UCHAGUZI wa kuwapata Viongozi wa Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Morogoro umehitimishwa huku Ndg. Selestin Mbilinyi ambaye ni Mkurugenzi wa Shule ya St. Patricia na Diwani wa Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro kushinda kwa jumla ya kura 37 na kuwabwaga wapinzani wake.
Uchaguzi huo umefanyika Machi 30/2024 kwenye Ukumbi wa DDC Mbaraka Mwishehe Manispaa ya Morogoro huku amani ikitawala kila kona kwa wagombea pamoja na wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa Wilaya.
Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi wa kutoka Chama Cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA) , Wakili Michael Mwambanga , ametangaza matokeo ambapo amemtangaza Ndg. Selestin Mbilinyi kama mshindi wa kinyang'anyiro kwa kura 37 kati ya kura 54 zilizopigwa.
Mara baada ya kushinda nafasi hiyo, Mbilinyi, amewashukuru wajumbe wa Mkutano huo kwa kumchagua kuwa Mwenyekiti huku akiwaahidi ushirikiano na kukuza Soko hususani upande wa soka la Shule na kuwa na ligi zenye ubora na mvuto kwa wapenda Soka.
" Wote tumeshinda hakuna aliyeshindwa sema ambao hawakupata nafasi hii ni kura hazija tosha lakini lengo letu ni kujenga nyumba moja kuhakikisha maendeleo ya Soka la Wilaya yetu ya Morogoro yanakuwa kwa kasi, tupeane ushirikiano tutimize yale ambayo tumeyaahidi kwa wanamichezo" Amesema Mbilinyi.
Wagombea wa nafasi ya Uwenyekiti na kura zao ni kama ifuatavyo, ambapo Ndg. Selestin Mbilinyi amepata kura 37, Ng'itu Godfrey kura 0 na Geofrey Mwatesa kura 17.
Aidha, wakili Mwambanga, amemtangaza ndugu Alfred Mdende maarufu kwa jina la Mteule kwa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu MRFA kwa kupata kura 38, huku Hamis Hassan Kiwenje kura 9 na Amiri Mussa Amiri kura 6.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa MRFA , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka Viongozi wa Vilabu wa Wilaya kutoa ushirikiano kwa Viongozi wapya ili watimize majukumu yao na kuleta matokeo chanya ya soko kwa Wilaya ya Morogoro.
Kihanga, amewataka viongozi wa Vilabu kuacha kusemeana maneno ya hovyo kwenye mitandao ya kijamii kwani kama wanaona hawaridhishwi na mienendo ya Viongozi wao zipo njia za kufuata kwa ajili ya kutaturiwa changamoto zao .
Post a Comment