Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAIDHINISHA KUTUMIA BILIONI 101,091,522.05 KWA MWAKA WA FEDHA 2024/2025


BARAZA la Madiwani Manispaa ya Morogoro imeidhinisha kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 101,091,522.05 katika mwaka wa fedha 2024/2025.


Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga katika  Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la kupitisha mpango na Bajeti ya Manispaa ya Mwaka 2024/2025.

Akizungumza juu ya bajeti hiyo, Mhe. Kihanga, amesema makadirio hayo yamepanda kwa asilimia 17.11 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2023/2024 ya shilingi 83,792,226,268.00.

Mhe. Kihanga ,amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Manispaa inatarajia kukusanya zaidi ya Bilioni 15,622,877,022.05 fedha za mapato ya ndani. 

Amesema kupanda kwa bajeti hiyo kumetokana na juhudi za makusudi za Manispaa kuongeza mapato na Serikali Kuu kujielekeza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema mpango wa bajeti ya mwaka 2024/2025 imejikita katika maeneo ya makusanyo ya mapato, elimu, uboreshaji wa miundombinu, afya, usafi wa Mji na utunzaji wa mazingira na Utawala bora na Mipango Miji.

Mchela, amesema upande wa divisheni ya utawala na rasilimali watu,  jumla ya shilingi 20,000,000/= zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa Jengo la Ofisi ya Kata ya Kingolwira.

Kwa upande wa kuwezesha wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kupitia fedha za asilimia 10 ya makusanyo, amesema hadi kufikia desemba 2023 imehamisha fedha jumla ya shilingi 448,177,035.79 kwa ajili ya mikopo ya kukopesha vikundi mbalimbali kwa vikundi vilivyokidhi vigezo vya kukopeshwa.

Upande wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Manispaa imeanza utekelezaji wa ujenzi wa machinjio ya kisasa Kata ya Mkundi kwa kutenga shilingi 150,000,000.00 fedha kutoka mapato ya ndani ambapo ujenzi huo upo kwenye hatua za ukamilishaji Jengo la kwanza  la kuchinjia pamoja na miundombinu mingine kwa awamu ya kwanza.

Kuhusu Sekta ya Mipango Miji na ardhi kupitia mapato ya ndani, jumla ya Shilingi 200,000,000.00 zimetumika kwa ajili ya upimaji na fidia na kuhamisha makaburi kupisha mradi wa TACTIC eneo la Tungi Tubuyu.

Sekta ya afya , Machela, amesema mwaka wa fedha 2023/2024 imepeleka jumla ya shilingi 333,622,895.00 kwa awamu tofauti kwa ajili ya kuendeleza , kukamilisha na kumalizia Zahanati 7 na Vituo vya afya 2 ikiwemo Zahanati ya Mazimbu, Mji Mpya, Kituo cha afya Tungi, Zahanati ya Kilakala, Zahanati ya uwanja wa Taifa, Kituo cha afya Mazimbu, Zahanati ya Kauzeni , Zahanati ya Mlapakolo ,  Zahanati ya Kiegea B pamoja na umaliziaji wa Choo cha Soko la Mji Mpya.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma, amesema Bajaeti ya Manispaa ya mwaka 2024/2025 asilimia kubwa inakwenda kuakisi kupunguza matatizo na changamoto kwa wananchi.

Kuhusu Miundombinu, Fikiri,ameitaka Manispaa kuwa na kikao cha pamoja na madiwani wote ambao wanachangamoto ya barabara na wadau wa barabara kujadili namna ya kuboresha barabara ili kurahisisha huduma hiyo ya usafiri kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amepongeza wataalamu kuandaa bajeti bora pamoja na kuwapongeza Madiwani kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.

DC Nsemwa, ametoa rai kwa wanaoishi maeneo ya mikondo ya maji kuhama mara moja ili kupunguza madhara ya mvua za elinino zinazotarajia kunyesha.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kufauata tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa afya.

Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Christine Ishengoma, amewataka wale ambao wamekopeshwa mikopo ya asilimia 10 na hawajarudisha warudishe mara moja ili kuweza kuruhusu mpango wa utaratibu  mpya wa mikopo kuendelea .


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.