WATOA HUDUMA VITUO VYA AFYA MANISPAA YA MOROGORO WATAKIWA KUTOA KIPAUMBELE UTOAJI ELIMU WA LISHE KWA WAJAWAZITO NA WAZAZI
MKUU wa Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Dkt. Maneno Matawa, amewataka Wataalamu wa huduma za afya wahakikishe suala la utoaji wa elimu ya lishe linakuwa kipaumbele kwa wazazi na wajawazito ili kupunguza uzao wa watoto wanaozaliwa uzito wa chini.
Hayo ameyasema katika mafunzo ya lishe kwa Vituo 63 vya kutolea huduma za afya Manispaa ya Morogoro kwenye Ukumbi wa Mji Mkuu Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Akizungumza na watoa huduma hao, Dkt. Matawa, amewataka watoa huduma hao kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha juu ya afya ya lishe kwa mama wajawazito pamoja na elimu juu ya malezi ya mtoto baada kuzaliwa na kuhakikisha mtoto ananyonyeshwa ndani ya miezi sita ya mwanzo.
Kuhusu suala la utapiamlo, Dkt Matawa, amesema sababu za utapiamlo katika jamii ni ulaji duni, maradhi, ukosefu wa chakula katika kaya, huduma duni za jamii, utunzaji duni wa makundi maalumu, ukosefu wa huduma za afya kwa jamii, na uchafuzi wa mazingira.
Aidha, Dkt. Matawa , Sambamba na hayo, amewataka pia kuliwekea mkazo suala la upimaji wa afya watoto na kuhakikisha watoto wanapimwa vizuri ili kuvumbua matatizo mengine yanayowakumba kutokana na ukosefu wa lishe bora kwani lishe bora hujenga vyema afya ya ubongo na mwili wa mtoto.
Mwisho Dkt. Matawa , amewataka watoa huduma kuweka msisitizo mkubwa kwa kwa Wazazi kuzingatia unyonyeshaji wa mtoto ndani ya miezi 6 ya mwanzo ili kumkinga na maradhi mbalimbali pamoja na kumjenga afya na akili .
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro, Ester Kawishe , amesema moja ya changamoto upande wa lishe ni baadhi ya wazazi kutozingatia umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo na wahudumu wa afya ya msingi kutokua na elimu ya kutosha ya upimaji wa maswala ya lishe.
Post a Comment