Header Ads

BILIONI 19 KUTEKELEZA MIRADI YA TACTICS MANISPAA YA MOROGORO


MANISPAA ya Morogoro inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 19, 606,559.46 kutoka Serikali Kuu kutekeleza miradi ya Tactics.

Ujenzi wa miradi hiyo utasimamiwa na Mtaalamu mshauri wa miradi kutoka Kampuni ya Ujenzi ya MHANDISI (Consultancy ) LTD  ambapo miradi hiyo itatekelezwa chini ya Ujenzi wa Kampuni ya M/s Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation.

Akizungumza katika utambulisho wa mradi huo Oktoba 23/2023 kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa , Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Winfred Kipako, amesema Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri 12 zinazotekeleza mradi huo kwa awamu ya kwanza.

Kipako,amesema Manispaa ya Morogoro itanufaika kwa ujenzi wa Barabara za Lami nzito zenye urefu wa KM 20.59 na Mifereji ya maji itakayoondoa mafuriko katikati ya Mji.

Aidha, amewataka wakandarasi na Mtaalamu mshauri kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi na kwa uzalendo kwa manufaa ya wana Morogoro.

“Wananchi mtahusika katika mradi huu niombe muwajibike ipasavyo ili kufanikisha utekelezaji wa mradi kwa ubora ,ufanisi (Value for money) kwa muda wa mkataba, najua wakandarasi mtakutana na changamoto niombe tuwe tunapeana taarifa kwa wakati ili mradi usikwame ” Amesema Kipako.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa ambayo itaifungua Manispaa na maeneo mengine 12 ya Mji ambayo  inatekeleza miradi kama hiyo.

“Niombe wananchi ambao mtapisha ujenzi huumara mpatapo malipo yenu mpishe kwa wakati mradi uende kadri ulivyo pangwa lakini wananchi niombe mlinde na kuitunza miundombinu ambayo Serikali inawekeza kwa fedha nyingi” Amesema Mhe. Kihanga.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Jeremiah Lubereje,  amewaomba wadau kama TANESCO ,MORUWASA na TTCL kuwa na mpango mkakati wa haraka wa kuondoa miundombinu ambayo itapitiwa na mradi ili utekelezaji ukamilike kwa wakati.

Lubeleje, amesema mradi huo utakuwa wa muda wa miezi 15 na utaanza utekelezaji Novemba 20/2023 na unatarajia kumalizika Februari 19/2025 huku kipindi cha matazamia ikiwa ni mwaka 1 na tarehe ya kukamilika kipindi cha matazamio ni Februari 18/2026.

Miongoni mwa miradi ya Tactic ni Ujenzi wa Barabara ya Muhimbili, Tubuyu II, Mjimwema, Barakuda, Kihonda-VETA na Ujenzi wa mifereji ya maji (ANT Mlaria na Kikundi).


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.