MABARAZA YA WAZEE YAZINGATIE VIPAUMBELE ILI KUCHOCHEA USTAWI NA MAENDELEO YA JAMII.
MRATIBU wa Wazee Manispaa ya Morogoro ,Hamisa Kagambo, ameyataka Mabaraza ya Wazee Manispaa ya Morogoro kuzingatia malengo ya Mabaraza hayo ikiwemo kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazo wakabili ili Kuchochea maadili mema, uzalendo na ushiriki katika shughuli za ustawi na Maendeleo ya jamii.
Kagambo,ameyasema hayo Oktoba 18/2023 akimwakilisha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Kata ya Mzinga.
Aidha,amesema Manispaa ya Morogoro itaendelea kufanya kazi kwa kushirkiana na Mabaraza hayo katika ngazi zote za Mitaa ,Kata na Wilaya.
"Tumeendelea kushirikisha Mabaraza ya wazee katika kufanya ufuatiliaji wa huduma mbalimbali na hata hili la bima ya afya nalo tayari tupo na mchakato wa kuendelea kufanya utambuzi wa wazee wanaostahili kupatiwa vitambulisho vya msamaha wa matibabu bure" Amesema Kagambo.
Kuhusu Mfuko wa TASAF amesema mfuko huo sio kwa wazee bali upo utaratibu ambao unatumika kuwaandikisha walengwa hivyo kama wapo walengwa maafisa Maendeleo ya Jamii wapo kwenye Kata wataendelea kuwatambua walengwa wa TASAF.
Aidha, Kagambo,amekumbusha wajibu wa wazee katika jamii hususani suala la maadili kwamba ni wakati wa kurejesha mifumo ya asili yenye kuchochea maadili mema katika jamii kwa sababu limekuwa ni changamoto.
"Wazee tumikeni kikamilifu kukemea yale yote yanayosababisha ukatili, unyanyasaji, unyanyapaa, mauaji katika jamii pamoja na mmonyoko wa maadili ambao unataka kuangamiza Vijana wetu" Ameongeza Kagambo.
Hata hivyo amewataka watu waache dhana potofu juu ya wazee kwani wazee ndio wanaowalelea watoto wao na kuongoza jamii katika maadili.
Diwani wa Kata ya Mzinga, Mhe. Salum Chunga, ameishukuru Manispaa na Menejimenti yake kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani kwa kuina Mzinga kwa kuwafikishia huduma za kijamii ikiwemo Ujenzi Majengo ya Zahanati, Ujenzi wa Shule ya Msingi na Sekondari.
Mhe. Chunga, amemshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha ambazo zimekamilisha ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ambayo itakuwa mkombozi wa wanafunzi kusoma karibu na maeneo yao na kuacha kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Mzinga, kwa niaba ya wazee ameomba suala la huduma za afya lishughulikiwe ili liwasaidie wazee kupata huduma sahihi na kwa wakati pale wanapopata matatizo.
Akitoa salamu za Baraza la Manispaa , Katibu wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro, Dkt.Basil Anga, ameipongeza Serikali kwa kuwajali Wazee kwani Vituo vya afya vina madirisha ya kutoa huduma kwa wazee.
Post a Comment