Header Ads

DC NSEMWA AWATAKA MADIWANI NA WATENDAJI WA KATA KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO ILI KULETA TIJA




MKUU wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Rebeca Nsemwa, amewataka Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Morogoro  kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi ya maendeleo   iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kujengwa kwa kiwango kinachohitajika.

Rai hiyo ameitoa Oktoba 26/2023 katika Kikao cha Baraza la Kawaida la Madiwani la robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Kuu Manispaa .

DC Nsemwa,amesema kuwa  kuna umuhimu wa Madiwani na watendaji kuwa  karibu na wataalamu wanaojenga miradi katika maeneo yao kwani wao ndio wasimamizi wakuu wa miradi hiyo.

Amesema kuwa Serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika miradi  hivyo lazima miradi hiyo iwe na viwango ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katika hatua nyengine, amewataka Madiwani na watendaji kusimamia maadili katika maeneo yao pamoja na kuendelea kupiga vita ukatili wa Kijinsia.


Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema ni wajibu wa Madiwani kwa kushirikiana na Watendaji wao hususani katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ili miradi hiyo iweze kuwa na manufaa kwa wananchi wao.

"Madiwani tushirikiane na watendaji wetu kama kuna kasoro kwa watendaji wetu  tunavyo vikao vyetu ndio sehemu yake ya kutatua migogoro yetu na sio kurumbana na watendaji jambo ambalo halina afya kwa maendeleo yetu" Amesema Mhe. Kihanga.

Katika hatua nyengine, Mhe. Kihanga, amelitaka Baraza la Madiwani kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kufikia malengo na kutimiza kiu ya Manispaa kuwa Jiji.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Ally Machela, amesema kuwa Ofisi ya Mkurugenzi inakuwa na imani kwamba Madiwani na Watendaji wa Kata ndio wasimamizi wakuu wa miradi iliyopo kwenye kata zao  hivyo ikitokea miradi haina kiwango ina maana viongozi ngazi ya Kata hawakutimiza wajibu wao.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.