Header Ads

DC NSEMWA AZINDUA KLINIKI YA ARDHI MANISPAA YA MOROGORO.

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amezindua Kliniki ya ardhi Manispaa ya Morogoro ikiwa na lengo la kuhakikisha migogoro ya ardhi inataturiwa kwa wakati  na kupelekea kupungua au kumalizika kwa migogoro hiyo.


Uzinduzi huo umefanyika Oktoba 23/2023 katika eneo la Ofisi ya ardhi iliyopo Stendi ya Daladala Mafiga huku mamia ya wananchi wakifurika kufuata huduma hiyo.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, DC Nsemwa, amewataka  Wananchi wa Manispaa ya Morogoro, kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na zoezi la Kliniki ya Ardhi.

“Kliniki yetu ya ardhi ina lengo la kuhakikisha wananchi wa Manispaa  ya Morogoro hawalii kwa sababu ya Ardhi, hay a ni maelekezo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona kwamba hataki kuona wananchi wanatoa machozi kwenye Ardhi ndio maana tumezindua Kliniki hii kuwashughulikia wananchi  migogoro yao” Amesema DC Nsemwa.

Katika uzinduzi huo, DC Nsemwa, amepata nafasi ya kumkabidhi mwananchi mmoja hati ya mfano kuashiria zoezi la Kliniki ya ardhi limezinduliwa rasmi.

Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Mohamed Lukwele ,amesema Kliniki hiyo ya ardhi itasaidia kutatua migogoro ya Ardhi kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wa Kamishina Msaidizi wa Ardhi  Mkoa wa Morogoro, Frank Minzkunte,  amesema ili eneo liweze kusajiliwa na kupatiwa hati ni lazima liwe kwenye mpango wa upimaji ardhi na lisiwe na mgogoro.

Minzkunte, amesema ili  kurahisisha zoezi la upimaji na utoaji wa hati za viwanja, ni muhimu wananchi kuepuka migogoro ya ardhi, huku akisisitiza suala la Wananchi kuzingatia  matumizi sahihi ya ardhi kwa kutokufanya kitu chochote kwenye ardhi kinachoweza kuwa kero kwa wengine.


Naye Msimamizi wa Sekta ya Ardhi Manispaa ya Morogoro, Bi. Emiline Kihunrwa, amesema zipo faida za umiliki ikiwemo dhamana ya mali isiyo hamishika kwenye baadhi ya mahitaji ya kisheria.

Kliniki ya Ardhi imewaweka pamoja wataalam wote wa sekta ya Ardhi kutoka Mkoani na Manispaa  ili kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi katika Manispaa ya Morogoro.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.