MBUNGE ABOOD AKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA VYENYE THAMANI YA MILIONI 17 SHULE YA SEKONDARI KINGOLWIRA NA LUKOBE
MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Dkt. Abdulaazi Abood, ametoa Kompyuta 6 kwa shule ya Sekondari Kingolwira na Kompyuta 6 Shule ya Sekondari Lukobe kwa ajili ya Masomo ya TEHAMA.
Ugawaji huo wa Vifaa vya TEHAMA katika shule hizo umefanyika Oktoba 30/31 2023 katika ziara yake ya kugawa vitendea kazi pamoja na vifaa tiba kupitia fedha za mfuko wa Jimbo.
Mhe. Abood, amesema ametoa Kompyuta hizo ikiwa ni mwendelezo wa zoezi lake la kutoa Kompyuta katika Shule za Sekondari Manispaa ya Morogoro ili kusaidia katika masomo ya TEHAMA.
“Nimetoa Kompyuta 6 , hizi hazipo kwenye bajeti ya mfuko wa Jimbo, lakini Kompyuta nyengine 6 ambazo zipo kwenye bajeti ya Mfuko wa Jimbo , nimekuwa nikitoa Kompyuta katika shule kwanza kukuza Teknolojia ya TEHAMA kwa watoto wetu, vifaa hivi thamani yake ni shilingi milioni 17,067,000/="Amesema Mhe. Abood.
Mwisho, Mhe. Abood, amewataka pia wananchi wa Jimbo la Morogoro waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwamba kupitia Rais pamoja na viongozi wa Chama, atazidi kuipaisha Jimbo la Morogoro Mjini na kufikia lengo lake la kuiletea maendeleo, kwa kuongeza miundombinu itakayochochea mzunguko wa fedha, fursa za ajira, mitaji, biashara na uwekezaji.
Naye Diwani wa Kata ya Lukobe, Mhe. Selestine Mbilinyi, amempongeza Mbunge Abood kwa kujali elimu na hata kutoa vifaa hivyo ambavyo vitasaidia wanafunzi katika masomo yao na kufanya vizuri Kitaaluma.
Nao baadhi ya Walimu ambao wamepokea vifaa hivyo kwa nyakati tofauti tofauti wamemshukuru Mhe. Abood, ambavyo vitakuwa msaada mkubwa kwao katika kuongeza ufanisi wa ufundishaji.
Post a Comment