WAKUSANYAJI WA TAARIFA ZA ANWANI ZA MAKAZI WATAKIWA KUZINGATIA MISINGI YA UTUMISHI WA UMMA.
WAKUSANYAJI wa Taarifa za Mfumo wa Anwani za Makazi Manispaa ya Morogoro wametakiwakuzingatia misingi ya utumishi wa Umma
Kauli hiyo ameitoa Afisa Tawala Wilaya ya Morogoro , Hilary Sagara akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Oktoba 06/2023katika ufunguzi wa mafunzo ya kujenga uwezo kwa washiriki wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi Manispaa ya Morogoro Ukumbi wa Mount Uluguru.
Sagara, amewaomba Wenyeviti wa Mitaa kwa kushirikiana na wajumbe wao waende kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo.
Pia, amesema Watendaji wa Kata na Mitaa wanayo dhamana ya kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa katika Kata na Mitaa yao na kuwataka wananchi wao wote wamefikiwa sambamba na kuongoza wakusanyaji taarifa na wataalam wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
"Vijana ambao mnakwenda kukusanya taarifa mfahamu kwamba mmepata nafasi ya kulitumikia Taifa lenu kwa vitendo , ni jukumu lenu kuhakikisha mnafanya kazi kwa bidii kulingana na mafunzo ambayo mmeyapata na ikizingatiwa kwamba baadhi yenu mlishiriki mazoezi ya nyuma hususani Operesheni Anwani za Makazi mwezi Februari hadi Juni 2022" Amesema Sagara.
Katika hatua nyengine, amesema kumekuwa na tabia baadhi ya wananchi kuharibu nguzo za majina barabara huku akitoa rai kwa yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja na Serikali haitasita kumchukulia hatua kazi za kisheria atakayebainika kufanya vitendo hivyo vyenye nia ovu.
Pia amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuwa Mbunifu na kuwa na mpango ambao utaufanya Manispaa ya Morogoro iendelee kuweka miundombinu ya Mfumo wa Anwani za Makazi huku barabara kuwa na vibao vyenye viwango vinavyoonesha majina ya barabara na kuwahimiza wananchi kujiwekea vibao vya namba za nyumba.
Kwa upande wa Mratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi Kitaifa, Eng. Jampyon Mbugi, amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya Anwani za Makazi 685,308 huku Manispaa ya Morogoro ikiwa na Anwani za Makazi 94,482zilizosajiliwa kwenye Mfumo wa Anwani za Makazi.
Post a Comment