WAZEE WATAKIWA KUWA MSTARI WA MBELE KUKEMEA VITENDO VYA MMOMONYOKO WA MAADILI.
MKURUGENZI wa Asasi isiyo ya kiraia ya Woman Of Substance chini ya Mkurugenzi wake , Mariam Mlembele, amewataka Wazee kuwaandaa na kuwalea vijana kwa ajili ya maisha ya uzeeni.
Mlembele, ametoa rai hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Oktoba 19/2023 kwenye Ukumbi wa Double M.
Aidha, Mlembele, amesema kutokana na mmomonyoko wa maadili ulioshamiri kwa sasa Wazee wana nafasi kubwa wakiwa ni viongozi wa familia kukemea vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii ya kitanzania.
"Sasa hivi tunapita kwenye kipindi cha mmomonyoko wa maadili, kwani umeenea ndani ya jamii nyingi, ni changamoto sana na sisi kama Wazee tusiposimama vizuri kwa nafasi yetu kubeba ulezi wa jamii tunaweza tukajikuta tunapata Wazee wa kesho na keshokutwa ambao watashindwa kulea vizazi vinavyokuja" Amesema Mlembele.
Hata hivyo, ameongeza kwamba, Mabaraza ya Wazee ni muhimu kwani ndio chombo ambacho kinatarajiwa kuwa mlezi namba moja wa kusaidia kukuza maadili kwa jamii.
"Katika zama hizi tunahitaji zaidi Wazee waendelee kufanya mengi ili kuambukiza vizazi vipya tabia njema na kuwezesha nao kufikia uzee ulio mwema lakini cha kusikitisha hivi karibuni kumekuwa na Wazee wanaoripotiwa kufanya matukio ya ajabu yasiyolingana na umri wao mfano kubaka na kulawiti watoto, kuwaoza watoto wadogo na kupandikiza imani mbaya" Ameongeza Mlembele.
Katika hatua nyengine , Mlembele, ,amesema atashirikiana na wanasheria wa Mkoa wa Morogoro ili kuweza kuwasiaida wazee kupata huduma za msaada wa kisheria wnapokuwa na changamoto zao.
Kwa upande wa Mratibu wa Wazee Manispaa ya Morogoro , Hamisa Kagambo, ameyataka Mabaraza ya Wazee kuendelea kushirikiana na kuwa na imani na Serikali yao kwani Serikali ipo pamoja nayo katika kuhakikisha inatekeleza afua mbalimbali kwa ustawi wa Wazee.
Kagambo,amesema Manispaa ya Morogoro inaendelea na juhudi za kuhakikisha Ustawi wa Wazee unaimarika ikiwemo kuimarisha mifumo ili wazee wapate huduma za kijamii kama Afya, ulinzi, usalama na matunzo kwenye makazi ya wazee.
Kuhusu mmomonyoko wa maadili, Kagambo,amesema kuwa Manispaa ya Morogoro imeshaandaa timu ya kamati ya maadili kupitia Baraza la Wazee la Manispaa kupita katika mitaa kwa ajili ya kutoa elimu .
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Mazimbu, Isack Wella, amesema kuwa ili wazee wajikwamue kiuchumi katika baraza lao wamepanga kuwa na miradi ya maurubai, viti vya plastiki, na Mahema ambavyo vyote vina gharama ya Shilingi Milioni 1 laki 6.
Wella, amesema Kata ya Mazimbu ina Wazee 700 katika Mitaa yote 7 ambapo kati ya wazee 402 ndio wameweza kupatiwa Bima ya Afya ya msamaha wa matibabu.
Wazee hao pia wameiomba Serikali kupitia Halmashauri zao watunge sheria ndogondogo ili kudhibiti ukiukwaji wa maadili katika jamii.
Pia, Wazee wa Mazimbu wameomba katika madhimisho ya mwaka 2024 Serikali iongeze huduma ya upimaji macho kwani asilimia kubwa ya Wazee wanasumbuliwa na macho.
Katika maadhimisho hayo , wazee 100 wameweza kupimwa magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na presha.
Akitoa salamu za Baraza la Manispaa la Wazee, Katibu wa Baraza hilo la Manispaa, Dkt.Basil Anga,amelipongeza Baraza la Mazimbu kwa maadhimisho mazuri huku akiwaomba Viongozi wa Mabaraza ya Kata na Mitaa ambao wanachangamoto za Uongozi wajitoe na kupisha Viongozi wengine kuongoza.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la kuhudumia Wazee Mkoa wa Morogoro, MOREPEO , Samson Msemembo, amesema MOREPEO ni Shirika ambalo lina shughulika na Changamoto za Wazee Mkoa wa Morogoro pamoja na kuwasemea wazee wote katika ngazi mbalimbali za Mitaa, Wilaya , Mkoa hadi Taifa.
Post a Comment