Header Ads

MGANGA MUU MANISPAA YA MOROGORO ATUMA SALAMU MABARAZA YA WAZEE

MKUU wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro, Dkt. Maneno Matawa, amesema Mabaraza ya wazee yabebe jukumu la kujadili changamoto zao ikiwemo kujua ni wazee wangapi ambao wanatakiwa kupewa Vitambulisho vya Msamaha wa  matibabu bure pamoja na utambuzi wa wazee wanaostahili kuingizwa katika mpango wa wanufaika wa TASAF.

Kauli hiyo,ameitoa Oktoba 18/2023katika Ofisi ya Kata ya Mzinga  akiwa katika kikao kazi mara baada ya kufanya ukaguzi wa ujenzi wa Majengo ya huduma ya kulaza wagonjwa Zahanati ya Konga Kata ya Mzinga.

Akizungumza katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na Diwani wa Kata hiyo na kamati yake  Dkt.  Matawa, amesema Manispaa inaendelea na jitihada mbalimbali ili kuendelea kuboresha huduma kwa wazee ambapo eneo la afya limepewa kipaumbele hasa Vitambulisho vya matibabu bure (ICHF) kwa wazee wasiojiweza.

Dkt. Matawa, amesema amefurahishwa sana na kuona Majengo hayo ya huduma yakiwa na Chumba maalaumu cha kuhudumia makundi mbalimbali ikiwemo kundi la wazee.

"Hii ni faraja kwetu kuona huduma zetu zinaendelea kuimarika, ni mara yangu ya kwanza kuja kukagua ujenzi huu tangia niwasili Manispaa hivi karibuni lakini nimeona kazi kubwa inaendelea kufanyika chini ya usimamizi wenu, sisi kama Manispaa tutahakikisha kuwa ujenzi wa Majengo haya yanakamilika kwa wakati ili yaweze kutoa huduma kwa wananchi" Amesema Dkt. Matawa.

Hata hivyo,ameipongeza Kata ya Mzinga pamoja na Kata zote ambazo zimefanya maadhimisho ya Mabaraza ya wazee huku akisema Mabaraza ya wazee ni muhimu yanatakiwa yapewe vipaumbele na kuwa endelevu.

Mwisho, amewataka Watendaji wa Kata kufanya utambuzi wa wazee kupitia Mabaraza yao ya Kata ili wapatiwe Vitambulisho vya msamaha wa matibabu na kupata huduma bila changamto yoyote katika vituo vya kutolea huduma za afya.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.