Header Ads

RC MWASSA AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUWAPATIA WAKULIMA MBOLEA YA RUZUKU


KATIKA  harakati za kukuza na kuinua sekta ya kilimo hapa nchini hususani ndani ya Mkoa wa Morogoro, wakulima wametakiwa kuendelea kujisajiri ili waweze kujiweka katika mazingira sahihi ya kupata mbolea ya ruzuku kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo 2023.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Abubakar Mwassa wakati wa ugawaji wa zawadi kwa washindi wa mbio za Kilimo Marathon pamoja na utoaji wa Tuzo za kilimo kwa washiriki mbalimbali tukio lililofanyika Oktoba Mosi mwaka huu 2022  katika Uwanja wa Jamhuri, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Mh. Mwassa amesema kuwa zoezi la kujisajiri ndio kigezo pekee kitakachowawezesha wakulima kupata mbolea za ruzuku kwa urahisi na kama mkulima hatajisajiri hatapata mbolea hiyo kwa wakati, hivyo amewataka wakulima wote kufanya jitihada za kujisajiri.

“wakulima wengi hawajajisajiri na wasipojisajiri watapoteza fursa ya kupata ruzuku ya mbolea, na mwisho wa kujisajiri ni Disemba mwaka huu” amebainisha Fatma Mwassa.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amefafanua kuwa Mkoa wa Morogoro una zaidi ya wakulima laki nne na elfu sabini (470,000) lakini mpaka sasa waliojisajiri ni wakulima asilimia 33 pekee.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huo amewaomba wanaMorogoro kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kudhamiria kwa dhati kuinua kilimo hapa nchini kkwa kutoa Ruzuku ya bei ya mbolea kwa takribani nusu ya bei iliyokuwa inauzwa awali, kwani amesema mfuko uliokuwa unauzwa shilingi 130,000 sasa utauzwa kwa shilingi 70,000 tu.

Hata hivyo, RC Mwassa,  ametumia fursa hiyo kuwaagiza Maafisa Kilimo Mkoani humo na wanahabari kusaidia kutoa taarifa hiyo kwa wakulima wajisajiri ili waweze kupata mbolea hiyo ya ruzuku.

Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa amewakaribisha wananchi wote kwenye tukio la uzinduzi wa msimu mpya wa kilimo 2023 tukio ambalo litafanyika Oktoba 4 mwaka huu Wilayani Kilosa Mkoani humo ambapo jumla ya Ekari 5,496 zitagawanywa kwa wananchi, emaeneo wanayopewa wananchi hao yanatoka katika mashamba yaliyofutiwa umiliki na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakizungumzia kuhusu Mbio hizo za Marathon, washiriki wa mbio hizo akiwemo Abraham Mwaikwila kutoka Ulanga wamesema utaratibu wa mbio hizo kipindi msimu ujao ni vema waandaaji wakagawa washiriki kulingana na umri wao, unaolingana yaani kuwepo na kundi la wazee  na vijana ili mshindi apatikane kwa haki kwa kuwa mtindo wa sasa mfano Mzee wa miaka 55 kwa vyovyote hawezi kumshindana Kijana wa miaka 20 au 25.

Mbio za Kilimo Marathon 2022 zimefanyika katika Viwanja vya Jamhuri, mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa, ambapo kivutio kikubwa kilikuwa mshindi wa kwanza km 5 kwa upande wa wanawake umenyakuliwa na mtoto wa umri wa miaka 10 Careen Charles Kajiru, anayesoma shule ya Msingi Benald Bendel  Mkoani Morogoro  ambaye amepata Medali na kufanya kuwa na jumla ya Medali 9 za mashindano mbali mbali ya mbio yakiwemo mshindano ya Selous Marathon, Kilimo Marathon pamoja na UMITASHUMTA huko Tabora.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.