DIWANI MBANDU AWATAKA WAZAZI KUWEKEZA KATIKA ELIMU
DIWANI Viti Maalum na Katibu wa Madiwani Manispaa ya Morogoro, Mhe. Salma Mbandu, amewataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwekeza katika elimu kwa kuwapeleka watoto wanaotakiwa kuanza shule na kuondokana na janga la kukosa elimu katika wilaya hiyo.
Mhe. Mbandu , ameyasema hayo , katika Mahafali ya Darasa la Saba Shule ya Msingi Kauzeni Manispaa ya Morogoro Oktoba 24/2022.
Aidha, Mhe. Mbandu, amesema kuna wazazi ambao wanashindwa kuwekeza katika elimu na kuwafanya watoto wao kujiingiza katika matukio hatarisha jambo ambalo sio zuri hivyo kila Mzazi aanze kuweka mikakati thabiti ya kumlea mtoto wake katika maadili na kumpatia elimu.
Hata hivyo, amesema kuwa maendeleo miongoni mwa jamii yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na kiwango cha uwekezaji katika elimu, ni vema jamii iwekeze kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu ili kujikwamua na umaskini uliopo na kupambana katika soko la ajira.
“Tukumbuke kwamba kuwekeza katika elimu ni mkakati wa muda mrefu unaohitaji dhamira, subira na kwamba matokeo yake huonekana baada ya muda mrefu wa uwekezaji na faida kwa wazazi mara baada ya mtoto kusoma na kuweza kumsaidia pindi azeekapo” Amesema Mhe. Mbandu.
Amesema kuwa, Manispaa ya Morogoro, ina rasilimali nyingi zinazohitaji viongozi wabunifu watakaohakikisha zinatumiwa vizuri kwa faida ya watu wote hivyo bila kuwekeza katika elimu rasimali hizo zitatumiwa vibaya na watu wasiojua faida ya elimu.
Ameongeza kuwa katika mipango ya Manispaa ya sasa ni kuhakikisha wanatatua changamoto za elimu pamoja na afya jambo ambalo limekuwa likifanyika na baadhi ya miradi imekuwa ikitumia fedha za mapato ya ndani katika kutekeleza hayo.
Mwisho, amewataka wazazi pia kuchangia suala la chakula shuleni kwani watoto wakikosa chakula viwango vya ufaulu vinashuka.
Post a Comment