WAZIRI JAFO APONGEZA MKOA WA MOROGORO KWA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, ameupongeza Mkoa wa Morogoro na wadau wa mazingira kwa ujumla kwa jitihada za kupambana na mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pongeza hizo amezitoa Oktoba 12/2022 katika maandamano ya amani kupinga uchomaji moto milima na uchafuzi wa mazingira Mkoani Morogoro maandamano yaliyofanyika Shule ya Sekondari Kilakala Manispaa ya Morogoro.
Dkt. Jafo ametoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, na Viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa mazingira kwa kushirikiana na wananchi kwa kushiriki kikamilifu kwenye utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali.
Pia amesisitiza kuongeza juhudi za kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kila mmoja kupanda miti na kuitunza kwa maendeleo endelevu.
Aidha, Amezitaka taasisi mbalimbali kama shule, vyuo, hospitali, magereza na maeneo mbalimbali kupanda miti na kufanya usafi ili kudumisha usafi na uhifadhi wa mazingira.
Amesema "mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na changamoto kubwa duniani, suala la ukame maeneo mbalimbali na mvua zisizotosheleza, jambo la kufanya ni kila mwananchi kufuata ajenda ya utunzaji wa mazingira na upandaji miti ili kufikia lengo la kupanda miti millioni 276.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mhe. Jabiri Makame, amesema ni wakati sasa kwa wadau wanaoshughulika na Mazingira kujitathmini na kufanyakazi kwa pamoja kwa kutoa elimu na uwezeshaji wa miche mbalimbali ya miti kwa jamii ili kuhakikisha jamii inawajibika vema katika suala la uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya sasa na ya baadae.
Kwa upande wa Mstahiki Meya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesisitiza suala la upandaji miti ili kurejesha hadhi ya Mkoa huo wenye asili ya kuwa na mazingira bora na yenye utulivu kwa binadamu na Wanyama hadi kupelekea uwepo wa mvua nyingi unaosababisha uwepo wa mito mingi inayotiririsha maji yake msimu mzima tofauti na ilivyo sasa.
Post a Comment