MBUNGE ABOOD KUSHUSHA NEEMA HII ZAHANATI YA KICHANGANI.
MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaazizi Abood, ameahidi kufanya upanuzi wa chumba cha kupumzikia wagonjwa katika Zahanati ya Kichangani Manispaa ya Morogoro.
Kauli hiyo ameitoa Oktoba 06/2022 wakati wa ziara yake ya kukabidhi Solar katika kutatua changamoto ya umeme katika Zahanati hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi Solar, Mhe. Abood, amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuboresha masuala ya afya hivyo wao kama viongozi wanaendelea kumuunga mkono Rais kwa kuwatumikia wananchi.
"Leo nimeleta hii Solar kusaidia umeme ukikata ili huduma ziendelee kutolewa, lakini nimeona nilichukue hili la upanuzi chumba cha kupumzikia wagonjwa maana chumba kilichopo ni kidogo" Amesema Mhe. Abood.
Mhe. Abood, amewaomba wananchi waendelee kushiriki katika shughuli za maendeleo huku akiahidi kuendelea kushughulikia kero za wananchi wa Jimbo la Morogoro mjini.
Upande wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Charles Mkumbachepa, amemshukuru Mbunge Abood huku akiahidi kushirikiana nae kupitia Ofisi ya Mkurugenzi katika kutatua kero za afya za Vituo na Zahanati.
Diwani wa Kata ya Kichangani, Mhe. Gilbert Mtafani, amemshukuru Mbunge na kumuahidi kumuunga mkono katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata ya Kichangani.
Post a Comment